• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 30, 2012

  SIMBA WAWAFUATA KIBABE MAAFANDE WANYONGE MOROGORO

  Wachezaji wa Simba SC

  Na Mahmoud Zubeiry
  SIMBA SC tangu inaondoka leo Dar es Salaam kwenda Morogoro tayari kwa mchezo wao dhidi ya Polisi mjini Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho, wakitoka kushinda mabao 3-1 dhidi ya Azam FC Jumamosi na kujiimarisha kileleni.
  Mabingwa hao watetezi juzi na jana walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Manzese, Dar es Salaam na kwa ujumla timu vizuri kuelekea mchezo huo wa tatu kucheza nje ya Uwanja wa Taifa, msimu huu baada ya awali kucheza mechi mbili Tanga dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT ambazo zote walilazimishwa sare ya bila kufungana.
  Simba imeshinda mechi zake zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoa sare mbili tu, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-1 na 2-2 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.
  Wekundu hao wa Msimbazi, wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 baada ya kucheza mechi 10, wakifuatiwa na wapinzani wao wa tangu enzi za bibi na babu, Yanga SC wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.
  Beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ wanaendelea kutumikia adhabu zao za kusimamishwa, lakini wachezaji wote wengine wapo fiti kabisa, ukiondoa Obadia Mungusa aliyefukuzwa mapema tu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
  Simba itamenyana na Polisi iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ambayo inashika mkia katika ligi hiyo, ikiwa haijashinda hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi hiyo zaidi ya kutoa sare mbili.
  Lakini hiyo haiifanyia Simba idharau mechi hiyo na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick ameanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya mechi hiyo.
  Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro- ni mbaya na kulingana na uzoefu walioupata wa kucheza kwenye Uwanja mwingine mbovu wa Mkwakwani, Tanga wanajua watakuwa na shughuli pevu keshokutwa.
  Hadi sasa Simba ndio timu pekee katika Ligi Kuu, ambayo haijapoteza mechi, ikiwa imeshinda mechi sita na kutoa sare nne, wakati Yanga imefungwa mechi mbili na Azam FC na Coastal Union zinazoifukuzia timu hiyo, zimefungwa mechi moja moja.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA WAWAFUATA KIBABE MAAFANDE WANYONGE MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top