• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 31, 2012

  YANGA KUPANDA KILELENI LIGI KUU LEO SIMBA IKITELEZA MOROGORO

  Wachezaji wa Yanga wakishangilia moja ya mabao yao katika Ligi Kuu msimu huu, shangwe hizi zitaendelea leo Uwanja wa Taifa?

  Na Mahmoud Zubeiry
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa nyasi za viwanja sita kuwaka moto kwa patashika ya michuano hiyo, ingawa macho na masikio ya wengi yatakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Taifa, Dar es Salaam, ambako wapinzani wa jadi katika soka ya nchi hii, Simba na Yanga watakuwa wanakipiga.
  Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Simba SC watakuwa wageni wa Polisi Morogoro, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, vigogo hao wakimenyana na timu zote ambazo zimepanda Ligi Kuu msimu huu.
  Toto Africans watamenyana na jirani zao  Kagera Sugar Uwanja wa Kirumba, Mwanza, JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa African Lyon Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, JKT Oljoro watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Mlandizi Pwani.
  Lakini mustakabali wa mechi kati ya Ruvu Shooting na Prisons haueleweki kwa sababu Prisons waliomba kuahirishiwa mechi hiyo baada ya kupata ajali wakielekea Tanga mwishoni mwa wiki kucheza na Mgambo JKT, jambo lililosababisha hadi mechi yao na Mgambo JKT iahirishwe pia.
  Simba wapo Morogoro tangu jana mchana tayari kwa mchezo huo, wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Azam FC Jumamosi na kujiimarisha kileleni.
  Mchezo huo utakuwa wa tatu kwa Simba kucheza nje ya Uwanja wa Taifa, msimu huu baada ya awali kucheza mechi mbili Tanga dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT ambazo zote walilazimishwa sare ya bila kufungana.
  Simba imeshinda mechi zake zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoa sare mbili tu, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-1 na 2-2 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.
  Wekundu hao wa Msimbazi, wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 baada ya kucheza mechi 10, wakifuatiwa na wapinzani wao wa tangu enzi za bibi na babu, Yanga SC wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.
  Beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ wanaendelea kutumikia adhabu zao za kusimamishwa, lakini wachezaji wote wengine wapo fiti kabisa, ukiondoa Obadia Mungusa aliyefukuzwa mapema tu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
  Bila shaka Milovan leo ataendelea na kikosi kile kile kilichoiadabisha Azam mwishoni mwa wiki; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi.
  Simba inamenyana na Polisi iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ambayo inashika mkia katika ligi hiyo, ikiwa haijashinda hata mechi moja tangu kuanza kwa ligi hiyo zaidi ya kutoa sare mbili.
  Lakini hiyo haiifanyi Simba kudharau mechi hiyo na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick ameiandaa vyema timu yake kwa ajili ya mechi hiyo.
  Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro- ni mbaya na kulingana na uzoefu walioupata wa kucheza kwenye Uwanja mwingine mbovu wa Mkwakwani, Tanga wanajua watakuwa na shughuli pevu leo.
  Hadi sasa Simba ndio timu pekee katika Ligi Kuu, ambayo haijapoteza mechi, ikiwa imeshinda mechi sita na kutoa sare nne, wakati Yanga imefungwa mechi mbili na Azam FC na Coastal Union zinazoifukuzia timu hiyo, zimefungwa mechi moja moja. 
  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga wanaoshika nafasi ya pili nao wako tayari kuendeleza wimbi lao la ushindi.
  Mshambuliaji Mrundi Didier Fortine Kavumbagu yuko fiti kuichezea Yanga SC katika mechi hiyo, baada ya kuibuka wasiwasi kidogo kufuatia kuvimba mguu baada ya mechi dhidi ya JKT Oljoro na kushindwa kufanya mazoezi juzi, lakini jana alifanya mazoezi na kumpa moyo kocha Mholanzi, Ernie Brandts kwamba anaweza kumtumia leo.
  Beki Kevin Patrick Yondan na mshambuliaji Said Rashid Bahanuzi nao wapo fiti kabisa na jana pia wamefanya mazoezi na wenzao kwa ukamilifu Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
  Kipa Said Mohamed Kasarama na kiungo Juma Seif Dion ‘Kijiko’ wanasumbuliwa na Malaria na hawatashiriki mechi hiyo ya leo, wakati mabeki Salum Abdul Telela, Juma Jaffar Abdul na Ibrahim Job Isaac wote bado majeruhi.
  Yanga iliyovuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha sasa imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutimiza pointi 20 katika mechi 10.
  Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
  Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, wanaweza kupanda kileleni leo, iwapo Simba itatoa sare au kufungwa na Polisi mjini Morogoro.
  Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Kwa ujumla, kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza matumaini ya ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni mtihani kwa Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’, walioshika nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.    
  Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
  Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia benchi.
  Wachezaji wa Simba wakishangilia moja ya mabao yao katika Ligi Kuu msimu huu, shangwe hizi zitaendelea leo Uwanja wa Jamhuri?
  Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna uwezekano mmoja wao atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea mwenzake baadaye. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: YANGA KUPANDA KILELENI LIGI KUU LEO SIMBA IKITELEZA MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top