• HABARI MPYA

  Sunday, October 21, 2012

  WANAFUNGWA BARCELONA TIMU BORA DUNIANI, KWA NINI ISIWE SIMBA?


  SIMAMISHA shabiki yoyote wa soka, popote kisha umuulize ipi ni klabu bora ya soka duniani, hakika kama wapo watakaokosea, hawatakuwa wengi, jibu litakuwa Barcelona FC ya Hispania.
  Na Mahmoud Zubeiry
  Pamoja na kucheza soka bora zaidi kuliko klabu yoyote duniani, Barcelona pia ndiyo timu yenye wachezaji bora zaidi duniani- yupo Messi ‘Mtu kutoka dunia nyingine’ aliyeshinda tuzo tatu mfululizo za Mwanasoka Bora wa Dunia tangu mwaka 2009.
  Messi ni mwanasoka wa nne kihistoria kushinda tuzo tatu za Ballons d'Or, na wa pili kushinda mfululizo mara tatu tuzo hiyo.
  Wanaye mwanasoka bora Ulaya, Iniesta na mafundi kibao katika timu- hii ni timu yenye msingi mzuri wa kuzalisha vipaji, kutafuta wachezaji bora, kuwatunza na kila kitu. Barcelona ni kila kitu.
  Kama yupo shabiki wa timu ambaye hata siku moja hawezi kuipenda  Barcelona atatoka Hispania na atakuwa shabiki wa kutupwa wa Real Madrid, lakini wengine wote duniani pamoja na kuwa na timu zao wanazozipenda, lakini wanaipenda pia na Barca kwa soka yao ya kuburudisha.
  Katika dunia ya leo ya soka nani hapendi kuwaona mafundi wa Barcelona akina Víctor Valdes, Dani Alves, Gerard Pique, Cesc Fabregas, Carles Puyol, Xavi Hernandez, David Villa, Andres Iniesta, Alexis Senchez, Lionel Messi, Thiago Alcantara, Jonathan dos Santos, Jose Manuel, Javier Mascherano, Marc Bartra, Sergio Busquets, Pedro Rodríguez, Jordi Alba, Martín Montoya, Adriano Correia, Eric Abidal, Isaac Cuenca, Alex Song na Marc Muniesa?
  Lakini pamoja na ubora wao, na wa wanafungwa na ndiyo maana hivi sasa si mabingwa wa Ulaya wala Hispania.
  Pamoja na ubora wao huo huo, hata kwenye Ligi ya Hispania hawapati ushindi kirahisi, mfano jana walishinda kwa tabu 5-4 dhidi ya Deportivo La Coruna.
  Messi alifunga mabao matatu katika dakika za 17, 42 na 76 na Jordi Alba akafunga dakika ya pili na Tello dakika ya saba, wakati mabao ya wapinzani wao yalifungwa na Pizzi kwa penalti dakika ya 25 na lingine dakika ya 46, Alex Bergantinos dakika ya 36, wakati Jordi Alba alijifunga pia dakika ya 78.           
  Hao ni Barcelona, jana wamefurahia ushindi wa 5-4 kwa sababu wameingiza pointi tatu La Liga. Kitendo cha kufungwa na mpinzani wako mabao manne, hata kama umeshinda matano, dhahiri huo ulikuwa mchezo ambao timu yoyote ingeweza kushinda.
  Lakini kwa Barca yaliisha jana na wanachokifanya ni kuangalia mbele, huo siyo mwisho wa soka katika klabu yao.
  Kwa nini Barca wanafungwa na wao ni bora? Kwa sababu wanafanya makosa, ndiyo maana wanafungwa. Kwa nini wanafanya makosa, kwa sababu soka ni mchezo wa makosa na makosa ndiyo yanatengeneza matokeo- bila makosa soka haitakuwa na ladha tena, kwa sababu timu zitakuwa hazifungani.
  Ndiyo maana, wengi duniani wanalaani mchezo wa ‘kijinga’ wa kucheza kwa kujihami, maarufu kama kubaki basi, ambao ‘mfalme’ wake ni Jose Mourunho, kocha wa Real Madrid.
  Chifu Omineokuma-Kile, mkufunzi wa marefa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwezi uliopita nilisoma waraka wake mmoja mzuri sana.
  Alisema; katika soka kwa tunalinganisha uwezo kwa uwezo (skill); kipaji kwa kipaji (talent) ndiyo tunaweza kutabiri matokeo. Sijui wachambuzi wa nyumbani huwa wanatumia vigezo gani, maana wakati mwingine huzungumza mambo ya dunia nyingine, tena siyo hata ile ya Messi.
  Chifu Omineokuma-Kile alisema kwa asili yake, soka imejipatia umaarufu ulimwenguni, kwa sababu makosa yanayotokea kwenye mchezo huo hayaleti furaha tu, bali na burudani kubwa pia.
  Katika dunia ya leo, ambayo mifumo ya uchezaji imeleta mabadiliko makubwa na kupunguza makosa kwa takriban muongo mmoja sasa kuna vitu vinawakera wapenzi wa mchezo huo, mfano mifumo kama ya Mourinho, lakini wengine wanaifurahia na hapo ndipo ilipolalia raha ya soka.
  Wewe fundi wa kucheza soka maridadi na kufunga mabao ya kusisimua, yule fundi wa kubana na kushambulia kwa kushitukiza kwa sababu ndicho alichokifanyia kazi kwenye mazoezi yake.   
  Namnukuu tena Chifu Omineokuma-Kile katika waraka wake; “Mabao hayawezi kufungwa hadi wapinzani walazimishwe kufanya makosa”.
  Kuna matatizo katika nchi yetu, viongozi wengi wa soka hawaijui soka na mbaya zaidi ni mashabiki na wamekuwa wakiwavuruga mno makocha. Hawajui, lakini wanajua kuliko makocha. Tatizo.
  Simba SC ilishinda mechi sita zote za mwanzo za Ligi Kuu, kabla ya kulazimishwa sare mbili mfululizo katika mechi zilizofuata.
  Katika mechi zote za awali Profesa Milovan Cirkovick alikuwa akitumia mfumo na wachezaji wale wale kama kulikuwa kuna mabadiliko katika kikosi cha kwanza yalikuwa madogo na kwa sababu kwa mfano kwenye mechi na Coastal mjini Tanga walikosekana, Emanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo ‘Redondo’.
  Baada ya sare ya pili, baadhi ya viongozi wa Simba wanaanza kumtilia shaka Milovan katika ufundishaji wake na upangaji wa timu. Sijui kama aina ya viongozi waliopo Simba wangekuwa na Barcelona pia, timu hiyo ingeitwa bora duniani. Sijui!
  Lakini viongozi wa Simba lazima wabadilike, lazima wajue kwanza, dira ya kocha wao ni ipi na watafute namna ya kuzungumza naye, bila kumtibua hata baada ya matokeo mabaya kwao.
  Ukocha ni kazi ngumu hasa kwetu huku Afrika ambako makocha wanaanza alifu kwa kijiti katika kufundisha wachezaji, tofauti na Ulaya ambako makocha wanafanya kazi na wachezaji ambao wako tayari na wanajitambua.
  Mwalimu anahitaji kupewa fursa afanye kazi yake kwa umakini na utulivu, bila kubughudhiwa- ili atengeneze timu itakayozalisha matokeo mazuri na kucheza soka ya kuvutia.
  Bado sijaiona timu inayocheza soka ya kuvutia katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu zaidi ya Simba SC.
  Wanaonana, wanazijua njia za mipira, wanacheza kwa kujiamini na hawapotei moja kwa moja mchezoni. Simba kama ilivyo Barcelona huwa wanafungwa kwa makosa na ilikuwa hivyo pia katika sare ya 2-2 na Kagera Sugar.
  Kuhoji kwa nini fulani hajapangwa, fulani kapangwa baada ya sare au timu kufungwa si sahihi, zaidi ya kumtibua tu kocha. Milovan amefanikikwa kumjengea kujiamini chipukizi Edward Christopher, kuna ubaya gani akifanya hivyo na kwa Haruna Chanongo?
  Basi, kwa sababu alipangwa siku ambayo timu ilitoka sare, hapo kocha alikosea kupanga timu. Hii si sahihi kabisa, lazima viongozi wetu wajifunze kuheshimu makocha na kuwapa muda.
  Kila napozungumza na Milovan, najifunza kitu, amelenga michuano ya Afrika. Anataka kuwa na timu bora yenye wachezaji wa kutosha, kabla ya Januari ili aweze kutimiza ndoto zake za kufika mbali kwenye michuano ya Afrika.
  Lakini kuna viongozi wake wanaangalia waliposimamia na hilo ndilo tatizo. Milovan alikuwa anamtumia Haruna Moshi kama mshambuliaji wa pili tangu msimu uliopita, lakini siku za karibuni amemrudisha kwenye nafasi ya kiungo na anataka sasa kutumia washambuliaji asilia ndiyo maana alijaribu kuwachezesha pamoja Felix Sunzu na Daniel Akuffo.
  Akuffo alipochemsha, Milovan alikasirika mno, kwa sababu alimtubilia mno mipango yake. Lazima tujifunze kuwa wapembuzi yakinifu na si wapiga soka kama jamaa zangu fulani, tujiulize Mserbia huyu anataka nini katika Simba?
  Kuwa na washambuliaji wawili, Sunzu na Akuffo au Abdallah Juma na pembeni ukawachezesha Okwi na Ngassa na bado unawatumia kwa pamoja viungo Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi, hii maana yake nini?
  Ni timu yenye kushambulia kwa kwenda mbele ndiyo ambayo anaitafuta Milovan na ili atimize malengo yake lazima awe huru na asiwe mwoga- lakini baadhi ya viongozi wanataka kumtibulia, tu kwa sababu hawataki timu ipoteze pointi.
  Kuna tangazo moja la sabuni, watoto wamecheza wamechafuka, anatokea mtu analalamika juu ya hali hiyo, lakini anaambiwa; wasipochafuka watajifunzaje? Basi na Milovan na Simba wasipokosea watajifunzaje? Jumapili njema!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: WANAFUNGWA BARCELONA TIMU BORA DUNIANI, KWA NINI ISIWE SIMBA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top