• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 23, 2012

  RAGE AOMBA UTULIVU SIMBA

  Rage

  Na Princess Asia
  MWENYEKITI wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
  Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
  Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.
  Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka Tanga na kuingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba SC itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo, ikitoka kulazimishwa sare ya tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0 na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
  Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
  Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: RAGE AOMBA UTULIVU SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top