• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 26, 2012

  WACHEZAJI WAVIVU YANGA WAWEKEWA MTEGO WA KUTEMWA, TIMU IKO SAWA KWA GWARIDE LA OLJORO KESHO

  Brandts akiwaongoza vijana wake mazoezini

  Na Mahmoud Zubeiry
  UONGOZI wa Yanga umemshauri kocha Ernie Brandts kutumia wachezaji wote badala ya kuwasahau kabisa wengine benchi, ili uweze kubaini wachezaji ambao hawana msaada katika timu na kuweza kuwatema katika dirisha dogo Januari, mwakani.
  Katika mechi za karibuni, Yanga ikiwatumia wachezaji tofauti wakiwemo wale ambao wamekuwa benchi kwa muda mrefu kama Nahodha Nsajigwa Shadrack, Nurdin Bakari na Rashid Gumbo.
  Yanga imeweka mtego kwa wachezaji ambao wanaridhika kupewa mishahara bure bila kufanya kazi na Januari watatupiwa virago.
  Chanzo cha habari kutoka Yanga kimesema kwamba, klabu inataka wachezaji washindani wa namba, ili kuongeza hamasa katika timu, badala ya kuwa na wachezaji wengi wa mazoezi tu.
  Yanga wanaonekana kucharuka sasa dhidi ya wachezaji wao kwa ujumla, kuanzia suala la nidhamu na uwajibikaji pia, baada ya kuona wanawekeza fedha nyingi katika usajili, lakini bado timu haichezi soka ya kuvutia, jambo ambalo wanaona linatokana na wahezaji kubweteka.
  Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb ‘aliwawakia’ wachezaji wa mbele wa timu hiyo kwa uchoyo wa pasi na kukemea tabia inayoonekana kuanza kujitokeza, wachezaji wa timu hiyo kutopendana.
  Bin Kleb aliingia ‘kwa hasira’ chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga na kuanza kufoka juu ya tabia hiyo, akisema timu inatengeneza nafasi nyingi, lakini kwa uchoyo wa baadhi ya wachezaji kutoa pasi kwa wenzao walio kwenye nafasi nzuri zaidi, inaambulia mabao machache.
  Bosi huyo alifanya hivyo baada ya mechi dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 3-0.
  Lakini pia Bin Kleb alimuuliza kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts kwa nini timu haichezi vizuri pamoja na kushinda. Brandts alitumia hekima kukwepa kujibu swali mbele ya wachezaji, lakini baadaye alimvuta pembeni Bin Kleb wakazungumza.
  Tayari kuna dalili za mgawanyiko ndani ya Yanga baina ya wachezaji na hilo lilijidhihirisha wakati Hamisi Kiiza alipofunga bao lake lililokuwa la tatu katika ushindi wa 3-0, hakwenda kushangilia na wachezaji wenzake, bali alimkimbilia kipa wa akiba, Mghana Yawe Berko kushangilia naye juzi.
  Ingawa hajawahi kulalamika, lakini ukiifuatailia Yanga tangu baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Kiiza ndiye ambaye mara nyingi amekuwa hapewi pasi na wenzake anapokuwa kwenye nafasi nzuri, ingawa yeye amekuwa anawapa tu wenzake pasi za mabao.
  Pamoja na hayo, hali hiyo inaonekana kidogo kuathiri uchezaji wa Kiiza, anayeonekana kuwa mnyonge na asiye na raha uwanjani na haikushangaza alipotolewa nje kipindi cha kwanza kwenye mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu.
  Lakini Kiiza amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu mno katika timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes pamoja na ‘kusuasua’ Yanga. 
  Yanga iko Arusha tangu jana na imefikia katika hoteli ya Joshmal, huku ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tayari kwa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya wenyeji JKT Oljoro kesho kwenye Uwanja huo.
  Yanga inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ikiwa na pointi 14, baada ya kucheza mechi tisa, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya kucheza mechi nane, wakati mabingwa watetezi Simba SC, wapo kileleni kwa pointi zao 19. Simba na Azam zitacheza kesho.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: WACHEZAJI WAVIVU YANGA WAWEKEWA MTEGO WA KUTEMWA, TIMU IKO SAWA KWA GWARIDE LA OLJORO KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top