• HABARI MPYA

    Wednesday, October 24, 2012

    YANGA YAZIDI KUNG'ARA LIGI KUU, AZAM YABANWA NA RUVU CHAMAZI

    Msuva kulia akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza. Kushoto ni Jerry Tegete na David Luhende

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Yanga itimize pointi 17, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kusimama katika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.   
    Ruvu walipata bao lao kupitia kwa Seif Abdallah na Kipre Tcheche akaisawazishia Azam.
    Uwanja wa Taifa, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na washambuliaji Simon Msuva na Didier Kavumbangu.
    Msuva alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya tano kabla ya dakika moja baadaye, Mrundi Kavumbangu naye kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo.
    Yanga ingekwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 kama mkwaju wa penalti wa Haruna Niyonzima usingegonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya mabeki wa Polisi kuondosha kwenye hatari.
    Refa Alex Mahagi kutoka Mwanza alitoa penalti hiyo, baada ya Msuva kuangushwa na beki John Bosco kwenye eneo la hatari wakati anakwenda kufunga.    
    Kipindi cha pili Yanga walirudi kwa kasi tena na kuendelea kulishambulia lango la Polisi, ingawa walipoteza nafasi nyingi na kutumia moja tu, dakika ya 58, mfungaji Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
    Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Coastal Union iliifunga 1-0 African Lyon Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Morogoro.
    Matokeo ya leo yanaziweka karibu mno, Simba, Azam na Yanga pale juu, kiasi kwamba ushindani na uhondo wa ligi hiyo unaongezeka.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Nahodha), Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na David Luhende/Nizar Khalfan.
    Polisi; Manji Kulwa/Kondo Salum, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmin Kissi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admin/Paul John, Paschal Maige, Mokili Rambo (Nahodha), Malimi Busungu na Nicholas Kabipe/Keneth Masumbuko.
    Katika mchezo wa awali wa utangulizi, Yanga B imeifunga TMK United ya Ligi Daraja la Pili, mabao 6-1 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na Polisi Morogoro.
    Mabao ya Yanga yamefungwa na Georgeb Banda matatu katika dakika za 61, 70 na 72, Hussein Moshi dakika ya 12 na Rehani Rehani dakika ya 19 na 27, wakati la kufutia machozi la TMK United, lilifungwa na Abdi Hashimu dakika ya 62.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA YAZIDI KUNG'ARA LIGI KUU, AZAM YABANWA NA RUVU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top