• HABARI MPYA

  Tuesday, October 23, 2012

  SIMBA SC SASA WAIGEUZIA KIBAO TFF, YANGA SAKATA LA MBUYU TWITE

  Hans Poppe

  Na Mahmoud Zubeiry
  SIMBA SC wamesema kwamba sasa inatosha kufanywa wajinga, wanataka kuwapa somo na Yanga ili wajue kwamba wao siyo klabu ya kuchezewa.
  Kufanya wajinga kivipi na wanataka kutoa somo gani?
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba wanakusanya vielelezo vya vyombo vya Habari juu ya mwenendo mzima wa sakata la beki Mbuyu Twite na kuvipeleka Mahakama ya Usuluhishi (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Kisa nini? Hans Poppe amesema ni ukimya wa TFF kutowapa rasmi taarifa ya hukumu ya pingamizi lao la Twite katika klabu ya Yanga na pia kushindwa hata kusimamia hukumu waliyotoa.
  Lengo nini? Hans Poppe amesema wanaamini kesi hiyo ikifika CAS, Twite atafungiwa kucheza soka na hata Yanga wataadhibiwa pia kwa kufanya kitendo kisicho cha kiungwana, kumsajili mchezaji ambaye tayari alikwishaini mkataba na klabu nyingine.
  “Sisi kama Simba hadi leo hatuna taarifa rasmi kutoka TFF juu ya hukumu waliyotoa katika kikao chao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji. Tumekuwa tukisikia tu kupitia vyombo vya habari, wakati sisi tuliwasilisha pingamizi letu kwa maandishi, naamini huu si utendaji sahihi,”alisema Hans Poppe.
  Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo ambaye ni Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba TFF pia iliamuru Yanga wawe wamekwishalipa fedha ambazo Twite alichukua Simba hadi kufika Oktoba 3, mwaka huu, lakini sasa mwezi huo unaelekea ukingoni na klabu yao haijalipwa.
  “Tunashindwa kuelewa hii ina maana gani, kwa sababu hukumu wametoa wao, na wao ndio wenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wake, lakini hadi leo Yanga hawajalipa na TFF pamoja na Kamati ya Sheria na Maadili wamekaa kimya, sasa sisi tunachukua hatua ambayo baadaye tusije kulaumiana,”alisema Hans Poppe.
  Alisema anashangaa TFF wamekuwa wepesi katika kusimamia na kutekeleza adhabu za Simba, kwa mfano barua barua ya hukumu ya mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi kufungiwa mechi tatu waliipata mapema tu baada ya kikao cha Kamati cha Ligi kupitia ripoti ya mechi ambayo Mganda huyo aliadhibiwa.
  “Tumekwishawaandikia barua ya kuwaomba hati ya hukumu siku nyingi, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa tunashindwa kuelewa nini lengo lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda, sasa wamejawa hofu na wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans Poppe.
  Septemba 10, mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka kulipeleka suala hilo CAS.
  Kamati hiyo, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
  “Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
  Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
  Kuhusu suala la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
  Hata hivyo, alisema kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
  Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
  Siku 21 walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua Simba, zilimalizika Oktoba 3, siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya Tanzania, walimenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoka sare ya 1-1.
  Simba walitarajia TFF ingeikata Yanga fedha hizo katika mapato yake ya mechi hiyo, lakini hawakufanya hivyo na hadi leo pia bado hawajalipwa na ndiyo maana wanaamua kupeleka vielelezo hivyo CAS.
  Mgongolwa aliwahi kuiambia BIN ZUBEIRY kwamba, kutokana na Yanga kushindwa kutekeleza agizo, hilo amemuagiza Katibu wa TFF aitishe kikao kingine cha Kamati hiyo ili kujadili hatua ya kuichukuliwa klabu hiyo kuwa kukaidi agizo hilo.
  Hata hivyo, yapata wiki mbili sasa tangu Mgongolwa amesema hivyo na hakuna dalili za Kamati yake kukutana kumaliza mgogoro huo.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA SC SASA WAIGEUZIA KIBAO TFF, YANGA SAKATA LA MBUYU TWITE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top