• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 29, 2012

  TFF YASAKA MILIONI 225 ZA KUIPELEKA MOROCCO SERENGETI BOYS

  Rais wa TFF, Tenga akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Kulia ni Sunday Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na kushoto, Katibu, Angetile Osiah 

  Na Mahmoud Zubeiry
  RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inahitaji zaidi ya Sh Milioni 225 kwa ajili ya kampeni yake iliyobakia ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika mwakani nchini Morocco.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya TFF, Ilala, Dar es Salaam, Tenga alisema kwamba shirikisho lake kwa sasa halina fedha hizo, kwa sababu hiyo haina mdhamini, zaidi ya kutegemea misaada ya wadau.
  Tenga alisema tayari Kamati ya Vijana ya TFF imekwishakutana kuweka mikakati ya kuiwezesha Serengti kushiriki vema kampeni hizo, ikiwemo kuunda Kamati ya kuisaidia timu hiyo.
  Hata hivyo, Tenga hakuitaja Kamati iliyoundwa kwa sababu bado hawajazungumza na Wajumbe walioteuliwa.
  Alisema kocha wa timu hiyo, Mdenmark Jacob Michelsen ameomba mechi za kujipima nguvu kabla ya kucheza na Kongo Brazaville kuwania tiketi ya Morocco na Kamati ya Vijana inahangaikia suala hilo kwa sasa.
  Alisema tayari kuna mwaliko kutoka Botswana wa Serengeti kwenda kucheza, lakini kutokana na ukosefu wa fedha wanashindwa hadi sasa kutoa jibu.
  Kikosi cha wachezaji 25 cha Serengeti Boys kipo kambini mjini Dar es Salaam tangu Oktoba 21, mwaka huu kujiandaa na mechi hiyo, ya kwanza ikichezwa nyumbani Novemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye.
  Tanzania imefuzu bila jasho hadi kufika hatua hiyo, baada ya wapinzani wake wa awali, Kenya na Misri kujitoa katika Raundi ya Kwanza na ya Pili.
  Kama Tanzania itafuzu kushiriki Fainali hizo za mwakani, itapoza machungu ya mwaka 2005 walipofuzu kucheza Fainali za Vijana wa umri huo kwa kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, lakini baadaye kwa sababu ya ‘kufoji’ umri wa Nurdin Bakari, ikaondolewa mashindanoni.
  Zaidi ya Fainali za Mataifa ya Afrika 1980 na CHAN 2009, katika soka ya wanaume, Tanzania haijashiriki fainali nyingine zozote za Afrika tangu iingie kwenye soka ya kimataifa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: TFF YASAKA MILIONI 225 ZA KUIPELEKA MOROCCO SERENGETI BOYS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top