• HABARI MPYA

    Sunday, October 21, 2012

    AKINA SAMATTA WANG'OLEWA AFRIKA, ILA REFA KAWAUMA SANA


    Na Mahmoud Zubeiry
    BAO la dakika ya 70 la M. Ben Mansour limezima ndoto za chipukizi wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kuwa Watanzania wa kwanza kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu yao Tout Puissant Mazembe kutupwa nje ya mashindano hayo na wenyeji Esperance ya Tunisia kwa jumla ya bao 1-0.
    Mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, TP Mazembe walilazimishwa sare ya bila kufungana mjini Lubumbashi.
    Kikosi cha Simba SC kilicheza Nusu Fainali ya michuano hiyo, wakati bado inaitwa Klabu Bingwa Afrika na kikatolewa na Mehallal El Kubra kwa mikwaju ya penalti, baada ya sare ya jumla ya 2-2.
    Lakini leo, wachezaji wawili wa Tanzania walikuwa wanajribu kuweka rekodi mpya, ikashindikana katika mchezo ambao, marefa walionekana dhahiri kuwabeba wenyeji.
    Hata bao lenyewe la ushindi ni la utata, kwani mfungaji alimvaa kipa Kidiaba Mutyata akiwa anaelekea kuudaka mpira na kuupiga kwa kuinua miguu kuusindikiza nyavuni. Kidiaba aliumia baada ya hapo na kutibiwa kwa zaidi ya dakika tano, lakini akashindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake ikachukuliwa na Matampi dakika ya 76.
    Alitoka uwanjani huku amefungwa kamba mkono, ambao uliumizwa katika purukushani hiyo. Pamoja na matokeo hayo, Mazembe watatakiwa kujilaumu wenyewe kwa kutocheza kwa utulivu, muda mwingi wakibutua mipira, jambo ambalo liliwapa kazi rahisi wapinzani wao kuwashambulia.
    Haikuwa Mazembe ile ambayo wengi wanaijua inayocheza kwa kujiamini, leo walicheza kwa kujihami zaidi- kana kwamba walikuwa wanataka sare na kwa bahati mbaya, bao hilo lilizima ndoto zao.
    Angalau baada ya kufungwa, Mazembe ilionekana kufanya mashambulizi ya kutafuta bao, lakini tayari wapinzani wao ‘wakapaki basi’ na hivyo kushindwa hata kuuingia ukuta wa Watunisia hao, ambao baada ya kupata bao la kuongoza walianza kupoteza muda kwa kujiangusha uwanjani.
    Samatta alikuwapo uwanjani tangu filimbi ya kwanza, lakini Ulimwengu aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Lusadisu.
    Esperance sasa ambao ni mabingwa watetezi, wanamsubiri mshindi wa kesho kati ya wenyeji Al Ahly ya Misri na Sunshine Stars ya Nigeria wakutane naye katika fainali. Mchezo wa kwanza Nigeria, Ahly walilazimisha sare ya kufungana mabao 3-3, hivyo wanapewa nafasi kubwa ya kukutana na Waarabu wenzao wa Afrika katika mechi ya mwisho. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AKINA SAMATTA WANG'OLEWA AFRIKA, ILA REFA KAWAUMA SANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top