• HABARI MPYA

  Wednesday, October 31, 2012

  TFF VIPI TENA KOMBE LA FA JAMANI?


  MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unaelekea ukingoni na hadi leo hakuna chochote kilichosemwa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu michuano ya Kombe la FA.
  Na Mahmoud Zubeiry
  Katika kalenda ya mwaka huu ya matukio ya TFF, michuano ya FA iliorodheshwa, lakini wasiwasi unaanza kuja kwa sababu hata Kombe la Taifa liliorodheshwa nalo halikufanyika pia na hadi sasa mustakabali wa michuano hiyo haueleweki.
  Sote tunafahamu soka ya Tanzania ni sawa na homa za vipindi ambazo zinacheza katika kiwango fulani kwa kupanda na kushuka.
  Huo ndio, ukweli na hilo linadhihirishwa na takwimu za viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinapotoka, Tanzania inapanda na kuporomoka, haina muendelezo wa kupanda.
  Mimi si muumini sana wa takwimu hizi za FIFA, ingawa zina maana na zinatoa hali halisi, lakini mara nyingine nchi nyingine zinapanda katika staili ya maji kupwa na maji kujaa.
  Katika miaka ya karibuni soka yetu ilipanda hadi tukashika nafasi ya 89, katika mwezi Desemba mwaka 2007, wakati bado Mbrazil Marcio Maximo ni kocha mkuu wa timu yetu ya taifa, Taifa Stars.
  Kwa sasa Tanzania ni ya 123, hii ikiwa ni miaka mitatu baadaye tangu tupande hadi ndani ya timu 90 zenye kiwango kizuri cha soka duniani.
  Sasa tunalekea wapi? Hilo ndilo swali la kujiuliza ikiwa matokeo ya karibuni ndio haya tunayoyashuhudia sasa, tumefikia hadi kufungwa na Timu B ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wetu wa nyumbani, kutoka kuwafunga washiriki wa fainali za Kombe la Dunia New Zealand.
  Tatizo letu si makocha na hata kama makocha ni tatizo kweli, ni vigumu kujua kwa sababu mfumo wetu ndio mbovu na hautoi fursa ya kuwa na wachezaji bora.
  Nchi nyingi za Afrika zinabebwa na nyota wao wanaocheza Ulaya, lakini sisi tunategemea zaidi wachezaji wa nyumbani na ambao watatoka kwenye Ligi Kuu tu.
  Kutoka kwenye wastani wa wachezaji 450 wanaocheza Ligi Kuu ya Bara isiyo na ushindani, inayonuka rushwa na uvundo wa uozo wa marefa wetu wasiojua, manazi na wala hongo ndio tunategemea kupata wachezaji wa kuunda timu ya taifa.
  Rejea msimu uliopita, ligi yenye timu 12 maana yake kila timu ilicheza mechi 22 na bingwa akapatikana. Katika wachezaji hao 400, inawezekana nusu yake tu walicheza japo mechi 20 za msimu, wakati kitaalamu ili mchezaji awe fiti, anatakiwa kucheza mechi zisizopoungua 40 kwa msimu.
  TFF pale wana Kurugenzi ya Ufundi, chini ya mwalimu aliyebobea tu Sunday Burton Kayuni ambaye sina shaka analijua hili, lakini je ametoa mwongozo utakaotuwezesha kuwa na mfumo bora na amepuuzwa au hajatoa? Wanajua wenyewe.
  Rais mwenyewe wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kitaaluma pia ni kocha na mchezaji mstaafu wa kiwango cha kimataifa, je hayajui haya?
  Tanzania tumekuwa watu wa kukariri kariri mambo, wengi sasa wanasema ‘youth’ na mashindano mengi ya vijana yameanzishwa, lakini je yanaendeshwa kwa malengo? Hapo kuna shaka.
  Klabu za Ligi Kuu zimeshinikizwa kaunzisha timu za vijana na sasa ni takriban mwaka wa nne, tujiulize vipi kuhusu maendeleo ya timu hizo za vijana?
  Tuna mashindano mengi ya vijana, lakini kutoka kwenye mashindano hayo mchezaji anaendelezwaje?
  Nchi nyingi duniani mbali ya kuwa na Ligi Kuu, zina mashindano mengine madogo yenye msisimko kama Kombe la Ligi, Kombe la FA na Super Cup. Pia wana Ligi za vijana madhubuti, mfano pale England ligi ambayo imemkomaza kiungo chupukizi Mtanzania, Adam Nditi akiwa na Chelsea.
  Uganda wana ligi hadi ya wachezaji wa akiba, ambayo imewasaidia mno kuwafanya wachezaji wao wengi wawe fiti, kwa sababu wasiocheza katika vikosi vya kwanza vya klabu zao, wanapata changamoto kupitia ligi hiyo.  
  Hakika mashindano haya yanaongeza msisimko wa soka katika nchi husika na wakati fulani yanafanya nchi iwe na bingwa zaidi ya mmoja.
  Birmingham City ‘The Blues’ ya England waliotaka kuzuru nchini mwaka jana kucheza na vigogo wa soka hapa nchini, Simba na Yanga, wakati huo walikuwa ni mabingwa wa Kombe la Ligi, ingawa wamekwishaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.
  Birmingham waliifunga Arsenal katika fainali ya Kombe la Ligi mabao 2-1, Mnigeria Obafemi Martins akifunga la ushindi, msimu ambao Manchester City walitwaa ubingwa wa Kombe la FA na Man United ubingwa wa Ligi Kuu.
  Hapa Tanzania, baada ya Ligi Kuu, watu wanasubiri mashindano ya ujanja ujanja tu ya watu kujitengenezea fedha, lakini hakuna tena mashindano mengine makubwa, zaidi ya hiyo michuano ya BancABC Sup8R iliyoanza mwaka huu na Simba B ikatwaa ubingwa.
  Faida ya mashindano ya ziada kama Kombe la FA ni kutoa fursa kwa wachezaji ambao hawana namba kwenye vikosi vya kwanza nao kucheza. Kwa mfano, Kombe la FA tutarajie hadi Friends Rangers ya Manzese na Ugimbi ya Kurasini zitacheza, maana yake sasa klabu za Ligi Kuu zitaweza kutumia wachezaji wake wa vikosi vya pili, jambo ambalo litasaidia kuwakomaza.
  Wakati umefika sasa, TFF ifunguke zaidi na kupanua wigo wa miundombinu ya kuinua soka ya nchi hii badala ya kuishia kufikiria tu kuwa na mashindano ya mpito pekee. Tunahitaji michuano zaidi ambayo mchezaji atacheza mechi zaidi ya 10 akionyesha umahiri ule ule.
  Mifano ipo, wachezaji kama Abuu Ramadhan ‘Amokachi’, aliyewahi kucheza Yanga kabla ya mizengwe kumuondoa kwenye soka angali mdogo, alitokea kwenye mashindano ya Kombe la FA wakati bado yanafanyika nchini, akiichezea Baker Rangers ya Magomeni.
  Ukweli ni kwamba Tanzania bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio na maana yake kazi kubwa inahitaji kufanyika, lakini ajabu TFF wanaonekana kuridhishwa na hali iliyopo.
  Tazama sasa Kombe la Taifa limekufa kifo cha kawaida, kutokana na kile ambacho sisiti kusema TFF kuzidiwa ujanja au kutokuwa na mitazamo ya mbali.
  Kombe la Taifa limekufa kwa sababu ya kukosa udhamini- baada ya mdhamini wake wa awali, Kampuni Bia  Tanzania (TBL) iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kuachia michuano hiyo.
  Wazi, TBL walijitoa Taifa Cup baada ya kupata dili la kujitangaza kupitia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo awali ilikuwa inadhaminiwa na kampuni nyingine ya Bia nchini, Serengeti (SBL).
  Mkataba wa udhamini wa Taifa Stars na SBL ulimalizika Desemba mwaka jana na TFF ikashindwa kukubaliana dau la mkataba mpya na SBL, na kuingia mkataba mpya naTBL. TFF waliuita mkataba huo ni mnono sana. Kweli kabisa, kwa sababu TBL walipanda dau, kutoka lile walilokuwa wakitoa SBL.
  SBL walianza kuidhamini Stars mwaka 2006, ikiwa haina na haijawahi kuwa na mdhamini. Katika kipindi hicho, SBL ilitekeleza vema mkataba wake wa udhamini na timu hiyo na kuonekana dhahiri kuvuka mipaka katika kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri na kujenga hamasa ya mashabiki kurejesha mapenzi kwa timu yao ya taifa.
  TFF walishindwa kusoma ishara za nyakati wakaingia kichwa kichwa kwa TBL na kuwapa  mkataba wa kudhamini timu ya taifa, hawakujua nini kitatokea mbele. TBL ipo kibiashara zaidi na daima wataendelea kuangalia maslahi yao zaidi juu ya kile wanachotoa, kama kitaendana na wanachopata- sijui TFF wanafikiria nini, lakini matokeo yake ndiyo haya, Kombe la Taifa ‘marehemu’.
  Sasa basi, TFF watuambie na kuhusu Kombe la FA kama ilikuwa ‘magumashi’ tujue, maana tumezoea usanii huu katika soka yetu. Ndiyo, watuambie tujue na ili tujue zaidi soka yetu inapoelekea. Jumatano njema.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: TFF VIPI TENA KOMBE LA FA JAMANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top