• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 30, 2012

  KAVUMBANGU 100% YANGA

  Kavumbangu

  Na Mahmoud Zubeiry
  DIDIER Fortine Kavumbagu yuko fiti kuichezea klabu yake, Yanga SC katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mgambo JKT, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mrundi huyo alivimba mguu baada ya mechi dhidi ya JKT Oljoro na kushindwa kufanya mazoezi jana, lakini amefanya mazoezi na kumpa moyo kocha Mholanzi, Ernie Brandts kwamba anaweza kutumika kesho.
  Beki Kevin Patrick Yondan na mshambuliaji Said Rashid Bahanuzi nao wapo fiti kabisa na leo pia wamefanya mazoezi na wenzao kwa ukamilifu Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
  Kipa Said Mohamed Kasarama na kiungo Juma Seif Dion ‘Kijiko’ wanasumbuliwa na Malaria na hawatashiriki mechi hiyo ya kesho, wakati mabeki Salum Abdul Telela, Juma Jaffar Abdul na Ibrahim Job Isaac wote bado majeruhi.
  Yanga iliyovuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na kupanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutimiza pointi 20 katika mechi 10, kesho inatarajiwa kuendeleza mawindo yake.
  Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
  Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, wanaweza kupanda kileleni kesho, iwapo Simba itatoa sare au kufungwa na Polisi mjini Morogoro katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
  Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Kwa sababu hiyo, Yanga wamechukua tahadhari ya kutosha kuelekea mchezo huo na tangu juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb amekuwa ‘akienda mbio’ kuhakikisha timu inashinda keshokutwa.  
  Kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza matumaini ya ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni mtihani kwa Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’, walioshika nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.    
  Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
  Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia benchi.
  Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna uwezekano mmoja wao atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea mwenzake baadaye. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAVUMBANGU 100% YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top