• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 26, 2012

  SIMBA TAYARI KULAMBA KONI ZA AZAM KESHO

  Kikosi cha Simba

  Na Princess Asia
  WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wanatarajiwa kurejea kesho Dar es Salaam wakitokea Zanzibar ambako waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa.
  Pamoja na Juma Nyosso na Haruna Moshi kusimamishwa, lakini wachezaji waliobaki wana morali ya hali ya juu na wamepania kushinda mechi ya kwanza kati ya nne, baada ya sare tatu mfululizo.  
  Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar katikati ya Ligi Kuu kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya Azam, maana yake wanaipa uzito huo mechi hiyo.
  Simba ilienda Zanzibar Jumanne, siku moja baada ya kurejea kutoka Tanga, ambako ililazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Mgambo JKT Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo.
  Matokeo hayo, yaliifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu.
  Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
  Baada ya sare ya Jumapili, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
  Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
  Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SIMBA TAYARI KULAMBA KONI ZA AZAM KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top