• HABARI MPYA

    Sunday, October 28, 2012

    KIUNGO MPYA MBRAZIL WA COASTAL AAHIDI TAMU TUPU

    Deangelis Gabriel Barbosa akiwa na mkewe, Zaira Caroiline na mtoto wao, Lara Barbos.

    Mashaka Mhando, Tanga
    KIUNGO mshambuliaji mpya wa Coastal Union anayetokea nchini Brazili,Deangelis Gabriel Barbosa mwenye umri wa miaka 27, aliyetua Tanga mwishoni mwa wiki na kuanza mazoezi na timu hiyo ameaahidi kuipa mafanikio ili iweze kushiriki mashindano ya kimataifa barani Afrika.
    Barbosa alitua jijini hapa akiwa pamoja na mke wake, Zaira Caroline na mwanae Lara Barbos na ameahidi kuipa mafanikio timu hiyo kwa kushirikiana na wachezaji wengine waliopo kwenye timu hiyo ambayo hivi sasa inafanya vizuri katika mechi zao mbalimbali.
    Katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, kiungo huyo amesema anatokea Mtaa wa Bahia katika jiji la Paulo Afonso nchini Brazil na amesema atacheza soka la kisasa kwa ajili ya kuipa heshima timu hiyo ndani na nje ya nchini kwa kuwa anathamini mchezo huo ambao ni kazi yake.
    Mchezaji huyo tayari ameanza mazoezi na wenzake na amesafiri na timu hiyo ambayo leo inacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam, Chamanzi, Dar es Salaam ingawa hatacheza kwa sababu viongozi wa Coastal bado wanakamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo kibali chake cha kufanya kazi nchini.
    Mchezaji huyo siku alipotambulishwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Steven Mgutto, alitaja timu mbalimbali alizochezea kuwa ni pamoja na klabu ya New Road ya Nepal, ambako alipomaliza mkataba wake ndipo amekuja Tanzania.
    Mguto alisema wameingia mkataba wa miaka miwili na mchezaji huyo na kueleza endapo kiwango chake kitakuwa kizuri watamuongezea mkataba mwingine.
    Barbosa alisema atahakikisha anatoa mchango wake mkubwa kwenye timu hiyo ili aweze kuipa heshima inayostahili ikiwemo kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ili timu hiyo iweze kushiriki mashindano makubwa.
    Awali, Katibu wa Coastal Union, Kassim El Siagi aliwataka wanachama pamoja na wapenzi wa timu hiyo, kuendeleza mshikamano uliopo ili kuweza kutimiza malengo yao waliojiwekea ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
    Siagi alizitaja klabu ambazo mchezaji huyo aliwahi kuzicheza ni Sports Club ya Paulo Afonso 2004, Maruinense Sporting Club 2006 za Brazil, Churuchill Brothers ya India 2007-2008, Santa Cruz ya PB Brazili, 2009 Flamengo ya Brazili, 2009-2010 Proham  Football Club ya Carribean na 2010 ya New Road Club ya Nepal.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIUNGO MPYA MBRAZIL WA COASTAL AAHIDI TAMU TUPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top