• HABARI MPYA

  Tuesday, October 30, 2012

  MIGAMBO WAIFUATA YANGA NA VIRUNGU VILIVYOITULIZA SIMBA MKWAKWANI

  Kikosi cha Mgambo JKT

  Na Mashaka Mhando, Tanga
  TIMU ya soka ya Mgambo JKT ya mjini Handeni mkoani Tanga, imeondoka leo mjini Tanga, ilikokuwa imeweka kambi kwenda Dar es salaam ambako kesho itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na wenyeji Yanga katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mgambo inayoshika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa kwa kuwa na pointi 10 ikiwa imecheza michezo tisa, imeondoka na wachezaji wake 22 na viongozi watatu kwa ajili ya pambano hilo ambalo timu hiyo ilisema kuwa inalichukulia kwa umakini mkubwa ili waweze kuibuka na ushindi kutokana na kujiandaa vilivyo.
  Kocha Mkuu wa timu hiyo Mohamed Kampira, alisema jana mjini hapa kwamba, Yanga waailichukulie kuwa watawafunga kirahisi katika mchezo huo badala yake wategemee kupata upinzani hasa kutokana na kwamba timu hiyo ya Mgambo imejiandaa kuibuka na ushindi ili waweze kukaa katika nafasi nzuri katika mzunguko huu wa kwanza.
  "Tunaondoka kesho asubuhi (leo) kwenda Dar es salaam, kama timu tumejiandaa vizuri na tunatarajia kuwapa wakati mgumu Yanga na kuishinda, wasitarajie mteremko, sisi ni timu na tunaamini kwamba tutaibuka na pointi zote tatu," alisema kwa kujiamini Kampira aliyevaa viatu vya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Stephen Matata aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kuanza vibaya kwa kufungwa michezo mitano mfululizo tangu kuanza kwa ligi hiyo.
  Kampira alisema hadi sasa wachezaji wake wamekuwa na ari kubwa ya kuibuka na ushindi na hakuna majeruhi wote wapo katika hali nzuri ya kupambana na timu hiyo inayousaka ubingwa mwaka huu kwa udi na uvumba na kwamba amewata mashabiki wa timu hiyo kuiamini kwa wachezaji watafanya kazi iliyokusudiwa.
  Mgambo JKT ambayo baada ya kumtimua kocha ilikuwa imeshikwa na kocha msaidizi Josepj Lazaro ambaye aliipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Morogoro, akaifunga Mtibwa Sugar bao 2-1 kwenye uwanja wa Manungu, ikaifunga Toto African bao 2-0 na ikatoka sare ya 0-0 na Simba mchezo ambao Kampira ilikuwa ni mchezo wake wa kwanza kukaa kwenye benchi la timu hiyo.
  Wakati huo huo, mashabiki wa klabu ya Coastal Union ya Jijini hapa, wameipongeza timu yao kwa ushindi walioupata juzi walipoifunga JKT Ruvu bao 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es salaam hatau ambayo walisema inatia faraja na wamewataka wacheji wazidi kuongeza bidii ili lengo la kumaliza ikiwa nafasi za juu litimie.
  Mmoja wa mashabiki hao Fred Tayasar alisema wamejisikia furaha ushindi huo lakini pia umewapa majonzi makubwa kwa mchezaji wao Nsa Job kuvunjika mguu katika pambano hilo hatua ambayo alisema wapenzi wa timu hiyo wanaangalia uwezekano wa kumchangia fedha kwa ajili ya kumpa ili aweze kujikimu katika kipindi atakachokuwa nje ya uwanja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MIGAMBO WAIFUATA YANGA NA VIRUNGU VILIVYOITULIZA SIMBA MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top