• HABARI MPYA

    Monday, October 29, 2012

    YONDAN, BAHANUZI WARUDI RASMI KAZINI YANGA

    Bahanuzi

    Na Mahmoud Zubeiry
    BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi waliokuwa nje ya Uwanja kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, leo wanatarajiwa kuanza programu rasmi ya mazoezi na wenzao baada ya kupata ahueni ya kutosha.
    Wachezaji hao wamekuwa wakifanya mazoezi mepesi kwa zaidi ya wiki moja baada ya kupata ahueni kidogo na sasa wamepona kabisa na leo kocha Mholanzi, Ernie Brandts anatarajiwa kuwajumuisha kwenye programu yake kamili, Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    Yanga imerejea kutoka Arusha, ambako Jumamosi ilivuna pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kupanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wakitimiza pointi 20 baada ya kucheza mechi 10.
    Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
    Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame sasa wanajiandaa na mchezo wao ujao wa ligi hiyo, dhidi ya Mgambo JKT Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Kwa sababu hiyo, Yanga wamechukua tahadhari ya kutosha kuelekea mchezo huo na tangu jana Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb amekuwa ‘akienda mbio’ kuhakikisha timu inashinda keshokutwa.   
    Kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza matumaini ya ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni mtihani kwa Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’, walioshika nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.     
    Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
    Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya Yondan kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia benchi.
    Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna uwezekano mmoja wao atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea mwenzake baadaye. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YONDAN, BAHANUZI WARUDI RASMI KAZINI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top