• HABARI MPYA

    Sunday, October 21, 2012

    SIMBA SC KUPAA ZAIDI LIGI KUU LEO?

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    MABINGWA watetezi, Simba SC leo wanashuka dimbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na wenyeji Mgambo JKT katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Simba SC wako mjini Tanga tangu juzi jioni kwa ajili ya mechi yao ya leo inayotarajiwa kuwa kali nay a kusisimua, kulingana na hali ilivyobadilika ghafla katika Ligi Kuu hivi sasa.
    Simba iliyoanza Ligi Kuu kwa kishindo, ikishinda mechi sita mfululizo, imelazimishwa sare katika mbili mfululizo zilizopita 0-0 na Coastal Union mjini Tanga na 2-2 na Kegara Sugar mjini Dar es Salaam na leo imepania kumaliza mdudu wa sare.
    Kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick amesema yeye na wachezaji wake wamejifunza jambo baada ya sare ya pili na Kagera Jumatano na sasa wataongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha matokeo hayo hayajirudii.
    Lakini Mgambo nayo, iliyoanza Ligi kizembe, imezinduka na kushinda mechi tatu mfululizo, tena moja ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1 wiki iliyopita kabla ya kushinda 2-0 dhidi ya Toto African mjini Tanga.  
    Simba ipo Tanga na wachezaji wake 24, ambao ni makipa; Juma Kaseja Juma, Wilbert Mweta William na Waziri Hamad Mwinyiamani, mabeki Nassor Said Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah Mrisho, Paulo George Ngalema, Koman Bili Keita, Pascal Ochieng Akullo, Hassan Hatibu Kondo.
    Viungo ni Jonas Mkude Gerrald, Ramadhani Chombo Redondo, Amri Kiemba Athumani, Abdallah Omar Seseme, Ramadhani Singano Yahya, Uhuru Selemani Mwambungu, Mrisho Khalfan Ngassa, Mwinyi Kazimoto Mwetula na Salim Abdallah Kinje na washambuliaji Abdallah Juma, Daniel Akuffo, Felix Mumba Sunzu, Edward Christopher Shija, Haruna Athumani Chanongo na Emmanuel Arnold Okwi.
    Waliobaki Dar es Salaam ni Haruna Moshi ‘Boban’ anayesumbuliwa na maumivu ya misuli, Haruna Shamte, anayeumwa goti, Kigi Makassy anayeumwa goti pia, Shomari Kapombe anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu na Juma Said Nyosso anayetumikia adhabu ya kadi (tatu za njano).
    Simba bado inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 17, baada ya kucheza mechi saba, wakati Yanga iliyocheza mechi nane ni ya tatu kwa pointi zake 14.  
    Katika mchezo wa leo, huenda Milovan akawapanga mabeki Komal Bil Keita kutoka Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kucheza pamoja kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu, kwa sababu Juma Nyosso na Kapombe hawapo wote.
    Mechi nyingine za leo, JKT Ruvu itaonyeshana kazi na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Chamazi, wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC KUPAA ZAIDI LIGI KUU LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top