• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 25, 2012

  NYOSSO AKISANUA SIMBA SC, BOBAN AAMUA KUTULIA, NGASSA, KAZIMOTO WATAZAMWA KWA JICHI LA TATU

  Juma Nyosso

  Na Prince Akbar
  SIMBA SC imekubali kuvunja mkataba na beki wake Juma Said Nyosso kulingana na maombi yake, na imemtaka afike kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kujadili suala hilo.
  Habari za ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba Nyosso amewasilisha maombi ya kuvunja mkataba na klabu hiyo, baada ya kushushwa kikosi cha pili, akidaiwa kiwango chake kimeshuka hivyo amepewa fursa ya kwenda kukiboresha.
  Lakini Nyosso mwenyewe ameona kama hastahili kushushwa timu ya pili na ameomba asitishiwe mkataba wake aondoke, jambo ambalo uongozi wa klabu umelikubali.
  Nyosso si kama anatuhumiwa kuhujumu timu, bali anaambiwa uwezo wake umeshuka mno na kwamba amekuwa akiigharimu timu katika siku za karibuni, hivyo amepewa fursa ya kwenda kupandisha kiwango chake.
  Adhabu kama hii amewahi kupewa mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez katika klabu ya Manchester City ya England msimu uliopita na aliitumikia vizuri hadi aliporejeshwa tena kikosi cha kwanza, ambako aliisaidia timu kumalizia msimu vizuri kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.   
  Mbali na Nyosso, kiungo Haruna Moshi Shaaban amesimamishwa kwa wiki tatu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na katika kipindi hicho atakuwa akipokea nusu mshahara.
  Boban ameamua kurudi nyumbani kwake kupumzika na mkewe hadi adhabu hiyo iishe ajue mustakabali wake, ila amesema anaonewa kwa sababu hakupewa nafasi ya kujibu tuhuma zake kabla ya hatua kuchukuliwa, ingawa amechukulia poa tu.
  Wakati huo huo, habari zaidi kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba Mwinyi Kazimoto Mwitula, Ramadhan Suleiman Chombo na Mrisho Khalfan Ngassa nao wanaangaliwa kwa ‘jicho la tatu’ juu ya mwenendo wao kwenye timu hiyo na kwa nyakati tofauti wote wamekwishaitwa kuhojiwa masuala mbalimbali.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: NYOSSO AKISANUA SIMBA SC, BOBAN AAMUA KUTULIA, NGASSA, KAZIMOTO WATAZAMWA KWA JICHI LA TATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top