• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 25, 2012

  BIN KLEB AWAWAKIA WACHEZAJI WACHOYO WA PASI YANGA, KIIZA AFICHUA MGAWANYIKO KATIKA TIMU

  Kiiza 

  Na Mahmoud Zubeiry
  MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb jana ‘aliwawakia’ wachezaji wa mbele wa timu hiyo kwa uchoyo wa pasi na kukemea tabia inayoonekana kuanza kujitokeza, wachezaji wa timu hiyo kutopendana.
  Bin Kleb aliingia ‘kwa hasira’ chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga na kuanza kufoka juu ya tabia hiyo, akisema timu inatengeneza nafasi nyingi, lakini kwa uchoyo wa baadhi ya wachezaji kutoa pasi kwa wenzao walio kwenye nafasi nzuri zaidi, inaambulia mabao machache.
  Bosi huyo alifanya hivyo baada ya mechi dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 3-0.
  Lakini pia Bin Kleb alimuuliza kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts kwa nini timu haichezi vizuri pamoja na kushinda. Brandts alitumia hekima kukwepa kujibu swali mbele ya wachezaji, lakini baadaye alimvuta pembeni Bin Kleb wakazungumza.
  Tayari kuna dalili za mgawanyiko ndani ya Yanga baina ya wachezaji na hilo lilijidhihirisha wakati Hamisi Kiiza alipofunga bao lake lililokuwa la tatu katika ushindi wa 3-0, hakwenda kushangilia na wachezaji wenzake, bali alimkimbilia kipa wa akiba, Mghana Yawe Berko kushangilia naye jana.
  Ingawa hajawahi kulalamika, lakini ukiifuatailia Yanga tangu baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Kiiza ndiye ambaye mara nyingi amekuwa hapewi pasi na wenzake anapokuwa kwenye nafasi nzuri, ingawa yeye amekuwa anawapa tu wenzake pasi za mabao.
  Pamoja na hayo, hali hiyo inaonekana kidogo kuathiri uchezaji wa Kiiza, anayeonekana kuwa mnyonge na asiye na raha uwanjani na haikushangaza alipotolewa nje kipindi cha kwanza kwenye mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu.
  Lakini Kiiza amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu mno katika timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes pamoja na ‘kusuasua’ Yanga.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: BIN KLEB AWAWAKIA WACHEZAJI WACHOYO WA PASI YANGA, KIIZA AFICHUA MGAWANYIKO KATIKA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top