• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 28, 2012

  AZAM YAZIPANDISHA TENA ULINGONI SIMBA NA YANGA LIGI KUU BARA

  Kiungo wa Azam, Himid Mao Mkami, akimtoka kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto Mwitula katika mechi ya jana ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba ilishinda 3-1.

  Na Mahmoud Zubeiry
  YANGA jana imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya Azam FC kufungwa na Simba SC mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku yenyewe ikishinda 1-0 mjini Arusha dhidi ya wenyeji JKT Oljoro.
  Maana yake sasa mwelekeo wa mbio za ubingwa wa ligi hiyo zimegeuka kidogo, Yanga ikiwa inaifukuza Simba sasa kileleni, kwa tofauti ya pointi mbili.
  Mwishoni mwa wiki ijayo, Yanga itacheza na Azam FC, mechi ambayo itatengeneza taswira ya namna mzunguko wa kwanza utakavyomalizika.
  Azam ikishinda inaweza kurudi nyuma ya Simba SC, lakini tofauti na hapo watu watasubiri kuona kati ya watani hao wa jadi, nani atamaliza mzunguko wa kwanza akiwa kileleni.    
  Kabla ya kucheza na Azam, Yanga itacheza Mgambo Shooting Jumatano, wakati Azam itacheza na Coastal Union Chamazi.
  Ligi Kuu sasa inazidi kunoga baada ya jana Simba kuzinduka kutoka kwenye wimbi la sare, baada ya kufanikiwa kuichapa Azam FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo, unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC inapromoka hadi nafasi ya tatu kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa, ikiipisha Yanga nafasi ya pili, ambayo imetimiza pointi 20 baada ya kuifunga JKT Oljoro.
  Mabao ya Simba jana yalitiwa kimiani na Emanuel Arnold Okwi mawili na Felix Mumba Sunzu Jr. moja, wakati la Azam lilifungwa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
  Hadi mapumziko, tayari Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1, Azam wakitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja.
  Dakika mbili baadaye, Sunzu aliisawazishia Simba, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
  Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto.     
  Kipindi cha pili Simba walirudi na moto wao na iliwachukua dakika tano tu kuhitimisha karamu yao ya mabao, baada ya Okwi kuwainua tena vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
  Mrisho Ngassa ndiye alikuwa nyota wa mchezo wa jana, kutokana na kuisumbua mno Azam, iliyomuuza kwa mkopo Simba miezi miwili iliyopita.
  Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga iliibuka na ushindi wa 1-0, bao pekee la beki Mbuyu Twite, hilo likiwa bao lake la tatu tangu ajiunge na timu hiyo kwenye ligi hiyo.
  Kwa ushindi huo, Yanga imetimiza pointi 20, baada ya kucheza mechi 10 na kupanda nafasi ya pili.
  Mechi nyingine za ligi hiyo jana, African Lyon ilitoka sare ya 1-1 Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Ruvu Shooting ikaifunga 2-1 Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
  Mechi kati ya Mgambo JKT na Prisons iliyokuwa ichezawe jana Uwanja wa Mkwakwani, Tanga imeahirshwa kutokana na wachezaji wa Prisons kupata ajali wakiwa njiani kuelekea Tanga.
  Ligi hiyo itaendelea leo kwa michezo miwili kati ya JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: AZAM YAZIPANDISHA TENA ULINGONI SIMBA NA YANGA LIGI KUU BARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top