• HABARI MPYA

    Sunday, October 28, 2012

    MBUYU TWITE ADHIHIRISHA THAMANI YAKE YANGA

    Twite alipowasili Uwanja wa Ndege kujiunga na Yanga Agosti mwaka huu

    Na Mahmoud Zubeiry
    NI beki, lakini anawazidi washambuliaji kwa kufunga mabao. Huyu ni Mbuyu Twite Banza, beki aliyesajiliwa msimu huu Yanga, kutoka APR ya Rwanda, ambaye jana alifunga bao lake la tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Pamoja na kufanya kazi nzuri ya ulinzi, akicheza beki ya kati kwa pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika kipindi hiki ambacho Kevin Yondan anauguza goti aliloumizwa na Haruna Moshi ‘Boban’, Oktoba 3, mwaka huu, Twite anasaidia sana na mashambulizi pia.
    Hupanda kusaidia mashambulizi na kutoa pasi nzuri, lakini pia huyo ndiye tegemeo la Yanga katika mipira ya adhabu hivi sasa.
    Ana mashuti makali na ndiyo maana kocha Mholanzi, Ernie Brandts ameamua kumfanya mtaalamu wake wa mipira iliyokufa.
    Wakati Yanga wanafurahia matunda ya Twite, wazi wapinzani wao wa jadi, Simba SC watakuwa wanaumia sana kumuona kijana huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akipiga mzigo wa uhakika Jangwani.
    Kwa nini waumie? Simba SC ndio waliokuwa wa kwanza kumsajili Twite baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame- wakimtuma Mwenyekiti wao, Alhaj Ismail Aden Rage kwenda kukamilisha usajili wake Kigali, Rwanda.
    Rage alikutana na Twite, wakazungumza na kukubaliana, akampa fedha dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 1,000 kwa ajili ya tiketi ya kuja Dar es Salaam. Rage alipogeuka tu, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb akamfuata Twite.
    Bin Kleb akafanikiwa kumbadili mawazo Twite na kuamua kurudisha fedha za Simba, ili aje Yanga, ingawa kidogo umafia ulitumika hapo.
    Hadi leo Simba wanadai fedha zao walizompa Twite na tayari TFF imeitaka Yanga irudishe fedha hizo.
    Sahau kuhusu yote yaliyopita, kitu ambacho Yanga wanajivunia kwa sasa ni kwamba, Mbuyu Twite ameanza kurudisha gharama zao za usajili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MBUYU TWITE ADHIHIRISHA THAMANI YAKE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top