• HABARI MPYA

    Thursday, October 25, 2012

    MKUTANO MKUU TASWA MWEZI UJAO

    Amir Mhando

    Na Prince Akbar
    CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), imefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini wa Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika tarehe ambayo itatangazwa rasmi.
    Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Kamati ya Utendaji ya TASWA ilikubaliana katika kikao chake mwezi uliopita kuwa Mkutano Mkuu wa TASWA mwaka huu uwe wa aina yake kwa kuwawezesha wanachama kukaa pamoja na kubadilishana mawazo na ikashauri ikiwezekana ufanyike nje ya Dar es Salaam kama hali itaruhusu.
    Amesema kutokana na hali hiyo, kikao kiliiagiza sekretarieti ya TASWA itafute mdhamini wa kufanikisha suala hilo na kwamba kama ikishindikana mkoani ifanyike Dar es Salaam lakini kuwe na mdhamini.
    Amesema tayari hilo limefanyika na mdhamini amepatikana, ambapo hatua ya mwisho ya mazungumzo na mdhamini itakuwa mapema wiki ijayo  na baada ya hapo itatangazwa tarehe rasmi.
    “Nichukue nafasi hii kuwaomba wanachama ambao hawajalipa ada zao wafanye hivyo kwa kuwasiliana na Mhazini wa chama au Mhazini Msaidizi ili waepuke usumbufu wa kushindwa kuhudhuria mkutano huo,”alisema Mhando.
    Wakati huo huo: TASWA imempongeza mwanachama wake, Boniface Wambura kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
    Mhando amesema TASWA imepokea kwa furaha uteuzi huo wa Wambura ambaye ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na inaamini ataendelea kufanya vizuri kama anavyotekeleza majukumu yake ya kazi ndani ya TFF.
    “Tangu Wambura aanze kazi ya Ofisa Habari wa TFF kumekuwa na mapinduzi makubwa yanayohusiana na mambo ya habari na katika hili waandishi wa habari za michezo nchini ni mashahidi wa hilo kwani amekuwa mtu sahihi kwao na amekuwa na ushirikiano mkubwa usio na kifani kwa wanahabari wenzake,”alisema.
    Mhando amesema kwa kuwa Wambura ni mwanachama hai wa TASWA, kwa kuteuliwa kwake huko ni faraja kwa chama na tunamtakia kila la heri ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake kwani hiyo ni ishara tosha kwamba kazi yake inaonekana na inathamanika.
    Wambura ameteuliwa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012, ambapo atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MKUTANO MKUU TASWA MWEZI UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top