• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 30, 2012

  POULSEN AVUTIWA NA VIPAJI ZENJI, LAKINI...


  1.       Kamati ya Ligi jana (Oktoba 29,2012) ilifanya kikao pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kujadili mambo kadhaa, likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia televisheni na radio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati ilifanya mazungumzo na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala yafuatayo:
  a-      kwamba uamuzi wa kuzuia vituo vya redio na televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi lakini una kasoro katika utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa vyombo vya habari na pia haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari kufanya maandalizi kwa kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.

  b-      Kwamba Kamati ya Ligi haijakataza redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya redio ambavyo vinataka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye hivyo bila ya kuweka matangazo ya wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa moja yatadhaminiwa, basi vituo hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.

  c-       Kwamba vituo vya redio vitakavyotaka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke mashindano hayo kuwa ni “Ligi Kuu ya Vodacom”.

  d-      Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kutangaza moja kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni lazima viingie mkataba na TFF ambao utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa, kituo cha televisheni cha Star TV hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo hiyo hadi hapo mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba huo utasainiwa kabla ya mechi za kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali kuendelea kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.

  e-      Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kuchukua picha kwa ajili ya habari zinaruhusiwa kufanya hivyo. Endapo kituo hicho kitaonyesha mchezo uliorekodiwa, hatua zitachukuliwa dhidi ya kituo hicho.

  f-       Kamati inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa lengo zuri la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoziwezesha klabu kujimudu kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom iendeshwe kwa ubora zaidi.

  Kim Poulsen
  2.       Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim Poulsen amerejea Dar es salaam baada ya kufanya ziara kwenye visiwa vya Pemba na Unguja ambako alishuhudia mechi sita za Ligi Kuu ya Grand Malta kuanzia Oktoba 19, 2012 hadi Oktoba 26, 2012 visiwani Zanzibar. Poulsen alishuhudia mechi baina ya Falcom na Bandari iliyoisha kwa Falcom kushinda kwa mabao 3-1 na pia mechi baina ya Duma na Bandari ambayo iliisha kwa Bandari kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Mechi hizo mbili zilifanyika kisiwani Pemba.

  Poulsen pia alishuhudia mechi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja ambako Mtendeni iliibwaga Chipukizi kwa mabao 2-1; Mundu na Jamhuri (0-1), KMKM na Zimani Moto (1-0); na Mafunzo dhidi ya Chuoni iliyoisha kwa Mafunzo kulala kwa mabao 3-0.

  Poulsen amefurahishwa na ziara hiyo na kusema kuwa ni kitu kizuri kwake na kwa soka la Tanzania kwa ujumla. Poulsen alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyopata visiwani Zanzibar na kukishukuru Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar (ZFA) kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wote akiwa Zanzibar.

  Hata hivyo, Poulsen alisema hawezi kueleza kwa sasa kama ameona wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha Taifa Stars, lakini akasema amevutiwa na viwango vya wachezaji wengi.

  3.       TFF inapenda tena kuihimiza klabu ya Yanga kumalizana na mchezaji wake wa zamani, John Njoroge Mwangi kabla ya Novemba 2, 2012 ili ijiepushe na adhabu kaili inayoweza kuchukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa barua ya FIFA, iwapo Yanga haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na kusiwepo na mawasiliano yoyote, shauri hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba 14, 2012 kutathmini hukumu iliyotolewa mapema Januari mwaka huu.

  4.       Mchezo namba 10 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baina ya Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto mjini Tabora Oktoba 31, 2012, sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni ambayo Morani walikuwa wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati wakitoka Kigoma ambako walicheza na Kanembo.

  5.       TFF inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo gazeti la Habari Leo na Daily News, vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga akisema kuwa amewataka watu wanaotaka kugombea uongozi wa shirikisho watangaze nia ili wapate kujadiliwa. Waandishi walioandika habari hiyo hawakumnukuu vizuri Rais Tenga wakati akizungumzia masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha maana nzima ambayo Ndg. Tenga alitaka iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira wa miguu. Rais Tenga alivitaka vyombo vya habari vianzishe mjadala utakaowashirikisha wapenzi wa mpira wa miguu ili waelezee wanatarajia nini katika miaka ijayo na hivyo kuwafanya viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi kwa utashi wa maoni hayo ya wananchi. Tunaelewa kuwa Rais Tenga ni muumini wa kuheshimu katiba, sheria na kanuni na hivyo hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka mchakato wa uchaguzi wa TFF kwa kuwataka wanaowania uongozi kutangaza nia sasa badala ya kusubiri muda wa kikanuni ufike. Ikumbukwe katika kikao chake na wahariri aliwahi kuulizwa swali kama hilo na akasema kuwa akijibu lolote atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kuwa itamaanisha anaanza kampeniu kabla ya muda. Ni vizuri waliohusika wakafanya masahihisho ili kuzuia habari zao kutafsiriwa tofauti na wadau wa mpira wa miguu na hivyo kuweka uwezekano wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

  6.       TFF imebadilisha tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa watu wanaotaka kugombea uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es salaam (DRFA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa kanuni. Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ilitangaza jana kuwa uchukuaji fomu ungeanza leo, lakini DRFA iliandikiwa barua jana kuelezwa kuwa mchakato huo sasa utaanza kesho na uchaguzi utafanyika Desemba 12, 2012.


  Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA utakuwa kama ifuatavyo:
  30/10/2012                                         Kamati ya Uchaguzi DRFA kutangaza uchaguzi na nafasi
  Zinazogombewa kwa mujibu wa katiba ya DRFA
  31/10/2012                                         Kuanza kuchukua fomu za kugombea uongozi
  04/11/2012                                         Mwisho wa kurudisha fomu ifikapo saa 10:00 alasiri
  05-09/11/2012                                   Kamati ya Uchaguzi DRFA kupitia fomu za waombaji uongozi na
  kutangaza matokeo na kubandika kwenye mbao majina ya waombaji uongozi.
  10-14/11/2012                                   Kutoa fursa ya pingamizi dhidi ya waombaji uongozi. Pingamizi
  ziwasilishwe kwa katibu wa Kamati ya Uchaguzi DRFA na
  wawekaji pingamizi wazingatie Ibara ya 11 (2) ya Kanuni za
  Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
  15-17/11/2012                                   Kujadili pingamizi, usaili na kutangaza matokeo ya usaili na
  kuwajulisha kwa maandishi.
  18-20/11/2012                                   Kukataa rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA

  21-25/11/2012                                   Rufaa kusikilizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kutangaza
  matokeo ya rufaa (Kama hakuna rufaa, Kamati ya Uchaguzi ya
  DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi wanazogombea
  na kuanza kampeni).
  26/11/2012                                         Baada ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya
  Uchaguzi ya DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi zao
  na kuanza kwa kampeni

  12/12/2012                                         Uchaguzi  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: POULSEN AVUTIWA NA VIPAJI ZENJI, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top