• HABARI MPYA

    Monday, October 22, 2012

    SIMBA YAREJEA DAR, SASA HASIRA ZOTE KWA AZAM

    Simba SC

    Na Princess Asia, aliyekuwa Tanga
    SIMBA SC imerejea Dar es Salaam leo mchana na inatarajiwa kuingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Simba SC itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo, ikitoka kulazimishwa sare ya tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0 na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo Jumatano inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
    Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
    Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.
    Katika mechi ya jana ya Simba na Mgambo, iliyochezeshwa na refa Athumani Lazi wa Morogoro, dakika 45 za kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu na zilionyesha kiwango kizuri, ushindani mkubwa- kwa ujumla ilikuwa burudani.
    Kipindi cha pili kadhalika pamoja na kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick kufanya mabadiliko akiwatoa Mrisho Ngassa na Amri Kiemba na kuwaingiza Edward Christopher na Salim Kinje, bado walishindwa kuifunga Mgambo iliyopanda Ligi Kuu msimu.
    Katika dakika 10 za mwisho, ilishuhudiwa Mgambo wakicheza kwa kujihami zaidi kutokana na presha kali ya mashambulizi ya Simba SC.
    Katika mechi hiyo, kikosi cha Mgambo kilikuwa; Godson Mmasa, Yassin Awadh, Salum Mlima, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Ramadhani Malima, Chande Magoja/Nassor Gumbo dk85, Mussa Ngunda, Issa Kandulu, Fully Mganga na Juma Mwinyimvua.
    Simba SC;Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Hassan Hatibu, Paschal Ochieng, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Salim Kinje dk88, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Edward Christopher dk 79.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA YAREJEA DAR, SASA HASIRA ZOTE KWA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top