KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa klabu ya Yanga kujaza nafasi zilizowazi za Kamati ya Utendaji unaendelea vizuri chini ya Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.
Taarifa ya TFF kwa BIN ZUBEIRY jioni hii, imesema kwamba Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepokea kutoka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga nakala za fomu za maombi ya uongozi wa klabu hiyo pamoja na nakala za vyeti vya elimu vya waombaji uongozi kama sehemu ya taarifa ya awali ya mchakato wa uchaguzi huo wa Julai 15, mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema Kamati ya Uchaguzi ya TFF imebaini kuwa baadhi ya waombaji uongozi wamewasilisha nakala za vyeti vya kuhudhuria masomo ya sekondari (Secondary School Leaving Certificate) badala ya nakala za vyeti vya kuhitimu masomo ya elimu ya sekondari (Certificate of Secondary Education).
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekwisha ielekeza Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuwataka wagombea wote kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(4) na (5) inayowataka wagombea wote kujaza Fomu Na.1 ya maombi ya uongozi na kuambatanisha nakala ya cheti cha Elimu ya Sekondari (Certificate of Secondary Education) kama ilivyoainishwa kwenye Fomu Na.1 kipengele Na.9.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuwashauri wagombea ambao vyeti vyao vimepotea wawasiliane na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa maandishi ili kupata ‘Statement of Examination Results’itakayotumwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupitia TFF kuthibitisha kuwa wamehitimu elimu ya kidato cha nne.
Uhakiki wa vyeti vya elimu ya sekondari vya waombaji uongozi hufanywa na NECTA na vyuo husika kwa elimu ya juu kwa chaguzi za wanachama wa TFF. Wanachama wote wa TFF wanatakiwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi.



.png)
0 comments:
Post a Comment