• HABARI MPYA

    Monday, June 25, 2012

    SIMBA WAREJEA DAR USIKU HUU GWARIDE KAMILI LAANZA KESHO TCC


    Wachezaji wa Simba SC, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege usiku huu

     Na Princess Asia
    KIKOSI cha Simba SC kilichokuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara mechi mbili za kirafiki kimerejea Dar es Salaam usiku huu kwa ndege ya Shirika la ATC na kesho kinatarajiwa kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe, kwa ukamilifu zaidi, kwa maana ya wachezaji wote kuanza kazi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 2:40 usiku huu, Kocha Msaidizi wa Simba SC, Hamatre Richard alisema kwamba ziara ilikuwa nzuri na timu ilicheza vizuri mechi zote.
    Hamatre ambaye ni Mganda aliwasifia wachezaji wapya wakiwemo kipa Hamadi Waziri na viungo Kiggi Makasy na Salim Kinje kwamba walionyesha kiwango kizuri na anaamini wataisaidia timu msimu huu.
    Aliwasifia pia wachezaji vijana waliopandishwa kutoka timu B kwamba walionyesha soka safi na anaamini watafika mbali. Lakini katika ziara hiyo Hamatre pia alivutiwa na kiwango cha hali ya juu, kilichoonyeshwa na kiungo Uhuru Suleiman.
    “Uhuru alikuwa Nahodha wa timu katika ziara yetu na kwa kweli alicheza vizuri mno mechi zote na alifunga bao zuri sana Mwanza,”alisema Hamatre.
    Mapema usiku wa kuamkia leo, Kocha Mkuu wa Simba SC, Milovan Cirkovick aliwasili kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa mapumziko, tayari kwa maandalizi rasmi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Simba, mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame, 1975, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa mashabiki wao wa huko.
    Katika ziara yao hiyo, Simba ilicheza mechi ya mwisho jana Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba mabao 2-0. 
    Katika mchezo wa jana, kiungo mpya wa Simba SC, Kiggi Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu ajiunge nayo mwezi huu kutoka kwa mahasimu, Yanga.
    Hata hivyo, bao hilo la Kiggi lilidumu kwa dakika 20 tu, kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai Wekundu na hadi kipyenga cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
    Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu tatu, mbali na Simba watakuwepo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC.
    Kiggi Makassy baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege
    Salim Kinje
    Nahodha wa Simba Kanda ya Ziwa; Uhuru Suleiman akiwa na kijana wake Samir Nasiri aliyekuja na mama yake kumpokea
    Viongozi; kutoka kulia Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Pamba, Ibrahim Maestro na Meneja Nico Nyagawa. Hawa wamevuna pointi nne Kanda ya Ziwa.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAREJEA DAR USIKU HUU GWARIDE KAMILI LAANZA KESHO TCC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top