• HABARI MPYA

  Ijumaa, Juni 29, 2012

  YANGA WAANZA KUIKACHA SIMBA MAPEMAAAA


  Yanga wakijifua ufukweni

  Na Prince Akbar
  SAA chache baada ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC kuthibitisha kushiriki michuano ya Ujirani Mwema, inayoandaliwa na Chaam cha Soka Zanzibar (ZAF), watani wao wa jadi, Yanga SC wameamua kujitoa.
  Mapema leo, Ofisa Habari wa Simba SC, aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba watashiriki michuano hiyo, kufuatia
  majadiliano baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya Ufundi ya Simba.
  “Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kujitoa wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano hii. Kombe la Ujirani Mwema lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo kwa sasa,” alisema Kamwaga katika taarifa yake, akimnukuu Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
  Saa chache zilizopita, BIN ZUBEIRY imezungumza na Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ambaye amesema wao hawawezi tena kwenda kushiriki kwa sababu wanahofia wachezaji wao kuumia kabla ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
  “Mara nyingi tunapokwenda kwenye michuano ya Zanzibar, wachezaji wetu huumia, hivyo tunahofia hilo lisijitokeze wakati tuna wiki mbili tu kabla ya kuanza kutetea Kombe la Kagame,” alisema Sendeu.
  Wakati michuano ya Ujirani Mwema inatarajiwa kuanza Jumapili visiwani Zanzibar, Yanga ikipangwa kufungua dimba na Jamhuri ya Pemba jioni ya siku hiyo, Kombe la Kagame linatarajiwa kuanza Julai 14, Yanga ikifungua dimba na Atletico ya Burundi.
  Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, awali walisema watacheza michuano hiyo, wakati Simba walikataa kuthibitisha mapema hadi wajadiliane.
  Wapembuzi wa mambo wanasema timu hizo, zinaogopa kukutana mapema kukiwa kuna uwezekano wa kukutana pia kwenye Kombe la Kagame, kutokana na jinsi ambavyo CECAFA huchezesha ‘karata’ zake.
  Yanga walikubali kushiriki awali, baada ya kuwasikia Simba wakisema hawawezi kuthibitisha mapema na bila shaka taarifa za mabingwa wa Kagame kujitoa kwenye michuano ya Ujirani Mwema ziliwavujia mapema Wekundu wa Msimbazi ndio maana wakathibitisha kushiriki.
  Na haitakuwa ajabu, Yanga ikisema imebadilisha uamuzi wake na kuamua kushiriki michuano hiyo, Simba wakasikika wakisema wanajitoa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAANZA KUIKACHA SIMBA MAPEMAAAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top