• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 24, 2012

  MNYAMA SIMBA NA TAI MWEKUNDU WA KAMPALA KAMBARAGE LEO


  Kikosi cha Simba kilicho ziarani Kanda ya Ziwa

  Na Princess Asia
  BAADA ya jana kuichapa Toto African ya Mwanza mabao 2-0 katika mechi kali ya kirafiki iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabingwa wa Tanzania, Simba SC leo wanashuka tena dimbani kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kumenyana na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’.
  Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga ‘Mr Liverpool’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo asubuhi kwamba tayari wako njiani kuelekea Shinyanga baada ya mechi ya jana.
  Katika mchezo wa jana Mwanza, Wekundu wa Msimbazi walianza pambano hilo kwa kasi na iliwachukua dakika 17 tu kuandika bao la kwanza lililowekwa kimiani na Uhuru Selemani aliyemalizia vizuri pasi ya Abdallah Juma.
  Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilikuwa inaongoza kwa bao hilo moja.
  Katika kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Abdallah Seseme na Hassan Khatib na nafasi zao kuchukuliwa na William Lucian (Gallas) na Jonas Mkude.
  Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwani katika dakika ya 48, Simba iliandika bao la pili lililofungwa na Salim Kinje, mchezaji mpya wa Simba aliyesajiliwa kutoka AFC Leopards ya Kenya.
  Kinje alifunga bao hilo akiunganisha moja kwa moja kutoka nje ya 18 pasi ya kichwa kutoka kwa Uhuru.
  Katika pambano la jana, wachezaji waliosajiliwa msimu huu walikuwa ni Waziri Hamad, Paulo Ngalema, Kiggi Makassy, Kinje na  Abdallah Juma.
  Wachezaji wawili wa kikosi cha vijana Simba maarufu kwa jina la U-20, Haruna Chanonga na Lucian pia walicheza mechi yao ya kwanza kwa kikosi cha wakubwa leo hii.
  Juni 24 Simba itaingia kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga kupambana na mabingwa wa soka wa Uganda, Express FC.
  SIMBA; Waziri, Hassan (Gallas), Ngalema (Omar Waziri), Obadia Mungusa, Haruna Shamte, Amri Kiemba (Edward Christopher), Chanonga, Seseme (Kiggi), Abdallah (Ramadhani Salum), Kinje na Uhuru.
  Wakati huo huo: Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic anatarajiwa kutua wakati wowote kuanzia sasa kutoka nyumbani, Serbia alikokuwa kwa mapumziko. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MNYAMA SIMBA NA TAI MWEKUNDU WA KAMPALA KAMBARAGE LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top