• HABARI MPYA

    Thursday, June 28, 2012

    FABREGAS ATUA LEO JANGWANI


    Niyonzima 'Fabregas'

    Na Prince Akbar
    KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Fadhil Hakizimana Niyonzima anatarajiwa kutua nchini leo, kutoka, Kigali alipokuwa kwa mapumziko, kujiunga na wenzake tayari kwa maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, Niyonzima amechelewa kufika kutokana na tiketi yake kumaliza muda wake, lakini tayari amebadilishiwa na leo atatua nchini.
    Aidha, Sendeu amesema leo Yanga itaendelea kujifua kwenye Uwanja wa Kijitonyoma, kufuatia Uwanja wa klabu hiyo, Kaunda kuharibika kwa mvua zilizonyesha Dar es Salaam hivi karibuni.
    Sendeu alisema mpango wa kuupata Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam, ambao ndio mzuri unaendelea na ukikamilika, wakati wowote timu hiyo itahamia hapo.
    Mabingwa hao watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame wapo kwenye maandalizi ya kutetea taji lao la michuano hiyo, ambayo inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29, mwaka huu Dar es Salaam.
    Timu nyingine mbili za Tanzania zitashiriki michuano hiyo, ambazo ni mabingwa wa nchi, Simba SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC.
    Yanga bado ipo kwenye mchakato wa kusaka Kocha Mkuu, baada ya mwishoni mwa msimu kumtupia virago Mserbia, Kostadin Bozidar Papic.
    Inaelezwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo na kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo na wakati huo huo inazungumza na chaguo mbadala, kutoka Ulaya iwapo itamkosa mwalimu huyo aliyeiwezesha Taifa Strars kucheza fainali za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
    Yanga imefanya usajili wa kusisimua, ikiwanasa wachezaji nyota kama kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Kelvin Yondan, wote kutoka kwa mahasimu Simba SC, beki Ladislaus Mbogo kutoka Toto African, viungo Frank Damayo kutoka JKT Ruvu, Nizar Khalfan aliyekuwa anakipiga Marekani na mshambuliaji Simon Msuva kutoka Moro United.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FABREGAS ATUA LEO JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top