• HABARI MPYA

    Sunday, June 24, 2012

    MANJI AWE BOSI YANGA, BORA MO DEWJI NAYE AGOMBEE SIMBA


    Na Mahmoud Zubrity

    HADI kufika mwaka 1975, klabu za Simba na Yanga zilikuwa tayari zina majengo mazuri, magari na hadhi kubwa- na wakati huo waliokuwapo waliotabiri miaka 20 baadaye klabu hizo zitakuwa mbali zaidi kimafanikio.
    Hayakuwa mafanikio ya kiuchumi tu, bali hata soka- hicho ndio kipindi ambacho Simba na Yanga zilikuwa moto wa kuotea mbali katika michuano ya Afrika.
    Yanga ilicheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 1969 na 1970, mara zote ikitolewa kwa mbinde na Asante Kotoko ya Ghana, wakati Simba ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa na Mehallal El Kubra ya Misri mwaka 1974. 
    Simba na Yanga ziliendelea kuwa tishio kisoka na kipindi hicho ilishuhudiwa zikifanya ziara za mafunzo Ulaya na Amerika.
    Ilitabiriwa miaka 20 baadaye, mambo yatakuwa mazuri zaidi kwenye klabu hizo, lakini kutoka mwaka 1975 hadi leo sasa ni miaka 35 imepita, hali ikoje Simba na Yanga?
    Ni mbaya, mbaya kabisa, majengo yamechakaa, magari hakuna tena zaidi ya yale ya msaada kutoka TBL, yanayotokana na mkataba wao wa udhamini. Yanga ambayo ilikuwa juu zaidi kwa kuwa na mabasi, majengo zaidi ya matatu, Uwanja wa Kaunda, sasa imebaki na jengo moja ambalo lilifanyiwa ukarabati hivi karibuni na Yussuf Manji, pale Jangwani, japokuwa tayari limeanza kuharibika.
    Uwanja wa Kaunda umechoka, umechakaa kwa sababu hauna matunzo na haufai kwa matumizi, zaidi Yanga wanautumia kwa mazoezi ya kuwachangamsha tu wachezaji kama kipindi hiki wanaanza kukusanyika, lakini siku mbili zijazo utasikia wako Loyola.
    Hakuna taarifa za uhakika kuhusu majengo mengine ya klabu kama lile la Mtaa wa Mafia, lile la Tandale na ile nyumba ya NHC ambayo awali aliishi Profesa Victor Stanslescu, baadaye Tambwe Leya, kabla ya Charles Boniface Mkwasa. Leo Yanga inaingia gharama kuwapangia nyumba makocha wake, wakati wana nyumba yao waliyopangishiwa na NHC pale Fire, wamepokonywa?
    Najaribu kutafakari hali ndani ya Yanga ingekuwaje kama asingejitokeza Manji mwaka 2006 na kujitolea kwa hali na mali kuisaidia klabu hiyo, kwa kweli sipati jibu mambo yangekuwaje.
    Aliingia baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya waandishi wa habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
    Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga na sasa ameamua kabisa kuwa Mwenyekiti.
    Wafadhili wamekuwa wakiingia na kutoka kwenye klabu hizi tangu miaka ya 1990 na wamekuwa wakisaidia mno, angalau Simba wamekuwa wakitumia vizuri fursa ya ufadhili, lakini kwa Yanga zaidi wamekuwa wakiwageuza ‘mabuzi’ tu wafadhili wao.
    Zama za ufadhili wa Azim Dewji, Simba ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, zama za ufadhili wa Mohamed Dewji, Simba ilicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, ikiitoa Zamalek iliyokuwa inashikilia taji. Haya sasa, Yanga watuambie walifanya nini wakati wanafadhiliwa na Abbas Gulamali kwa pamoja na Murtaza Dewji au wakati huu wanaogelea kwenye bwawa la fedha za Manji, wanafanya nini?
    Narejea nyuma miaka ile Yanga iko chini ya Mwenyekiti Mangara Tarbu namna ilivyopata mafanikio ya haraka ya uwanjani na kiuchumi kama Simba ilipokuwa chini ya akina Mwenyekiti Dumelezi na Katibu Mkuu Said Mpolaki, naona kabisa kizazi kipya kimeshindwa kuzivusha katika hatua nyingine klabu hizi.
    Binafsi sijali kujiongezea watu wa kunichukia kwa kuandika ukweli juu ya soka ya nchi hii na sitarudi nyuma; wamepita watu wengi ndani ya miongo hii miwili, lakini hakuna chochote kilichofanyika na kila siku kinachojitokeza ni afadhali ya waliokuwapo.
    Umefika wakati serikali iingilie kati kuziokoa hizi klabu, kwani ni rasilimali za taifa hizi iwapo zitatumika vizuri. Zitatoa ajira kwa vijana, zitachangia pato la taifa kwa kodi, ikiwa tu zitakuwa chini ya usimamizi imara wenye tija.
    Leo Waingereza wamekubali timu zao zimilikiwe na wageni na sasa timu zote kubwa zinamilikiwa na wageni, lakini kwa sababu wenyewe haswa wenye timu wanachotaka ni furaha, wanaangalia mambo ya msingi mawili; klabu inanufaika kiuchumi, inapata mafanikio uwanjani? Inatosha.
    Manchester United, ama Chelsea FC, au Arsenal hata Liverpool, hazina makomandoo. Hazina ombaomba wa kuomba fedha viongozi. Hazina watu wanaolilia wapewe nafasi ya kuuza tiketi wala kusimama milangoni. Zina watu ambao wanataka ushindi na kusikia klabu inaigiza fedha.
    Hata kwetu Tanzania, mashabiki wa kweli wa timu hizi ni wale wanaonunua tiketi kwenda uwanjani kushangilia timu zao. Wanachotaka ni ushindi na kusikia klabu zao zinapata mafanikio na kuwa sawa na klabu nyingine zilizopiga hatua kubwa kiuchumi na kisoka Afrika.
    Lakini inasikitisha kuona miongo miwili imekatika Simba na Yanga zinazidi kutumbukia kwenye dimbwi la umasikini wa soka na uchumi, kwa sababu gani tusiwakumbuke akina Mangara na Dumelezi, waliozijengea klabu hizi misingi imara ya kisoka na uchumi? Wakubwa wa leo wanabadilisha suti na magari ya Kijapani, lakini klabu zinanuka uvundo, zinatia kichefuchefu. Wapo kwa ajili ya kusaka umaarufu tu, hawana cha maana wanachofanya.
    Angalau sasa Manji anaingia pale Yanga, naamini atasababisha mabadiliko makubwa na nitafurahi Mohamed Dewji naye akigombea Uenyekiti Simba katika uchaguzi ujao, kwa sababu atasaidia mno kuimarisha klabu hiyo na upinzani wa jadi wa klabu hizo, ambao ni chachu ya msisimko wa soka yetu. Alamsiki!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI AWE BOSI YANGA, BORA MO DEWJI NAYE AGOMBEE SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top