• HABARI MPYA

  Wednesday, February 06, 2019

  MAREFA WA SUDAN KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA NA AL AHLY JUMANNE IJAYO DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limewateua marefa wa Sudan kuchezesha mechi ya Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji, Simba SC na Al AHly Jumanne ya wiki ijayo kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Hao ni Simba Mahmood Ali Mahmood Ismail atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Waleed Ahmed Ali na Ahmed Nagei Subahi.
  Simba SC watakuwa wenyeji wa Al Ahly Februari 12 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Mchezo huo utafanyika siku tisa tu tangu Simba ichapwe 5-0 na Al Ahly Jumamosi ya Februari 2, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria, Misri mabao ya Amr Al Sulaya dakika ya tatu, Ali Maaloul dakika ya 23, Oluwafemi Junior Ajayi dakika ya 31 na Karim Nedved mawili, dakika ya 33 na 40.
  Mchezo mwingine wa Kundi D siku hiyo kati ya JS Saoura na AS Vita Uwanja wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar nchini Algeria utachezeshwa na marefa kutoka Rwanda, Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Ambroise Hakizimana na Justin Karangwa.
  Ikumbukwe mechi ya kwanza baina ya timu hizo ilimalizika kwa kwa sare ya 2-2 Uwanja wa Martyrs de la Penteccte mjini Kinshasa, AS Vita wakitangulia kwa mabao ya Kazadi Kasengu dakika ya 14 na Jean-Marc Makusu Mundele dakika ya 37, kabla ya JS Saoura kusawazisha kupitia kwa Mohamed El Amine Hammia kwa penalti dakika ya 45 na Sid Ali Yahia Cherif dakika ya 88.
  Baada ya mechi za mzunguko wa kwanza, Al Ahly inaongoza Kundi D kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na AS Vita yenye pointi nne, Simba SC pointi tatu na JS Saoura wanashika mkia kwa pointi zao mbili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAREFA WA SUDAN KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA NA AL AHLY JUMANNE IJAYO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top