• HABARI MPYA

    Tuesday, December 04, 2018

    SIMBA SC WAIFUMUA MBABANE SWALLOWS 4-0 MANZINI NA KUBISHA HODI HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

    Na Mwandishi Wetu, MANZINI
    SIMBA SC imeingia hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji, Mbabane Swallows jioni ya leo Uwanja wa Mavuso mjini Manzini, Eswatini, zamani Swaziland.
    Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1, baada ya kushinda 4-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya mchujo Jumatano ya wiki iliyopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Nelson Emile Fred atakayesaidiwa na washika vibendera Hensley Danny Petrousse na Gerard Pool, wote wa Shelisheli, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.



    Na yote yalifungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama dakika ya 28 na 33 na kipindi cha pili wachezaji wengine wawili wa kigeni Mganda Emmanuel Okwi na Mnyarwanda Meddie Kagere wakaunenepesha ushindi wa Simba.
    Okwi alifunga alifunga dakika ya 52 na Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tu tangu asajliwe Simba SC akitokea Gor Mahia ya Kenya akafunga dakika ya 63.  
    Simba SC sasa itakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya UD Songo ya Msumbiji na Nkana FC ya Zambia zinazorudiana kesho Uwanja wa Nkana mjini Kitwe.
    Mchezo wa kwanza, Nkana FC timu anayochezea beki wa zamani wa Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam, Hassan Kessy ilishinda 2-1 ugenini Uwanja wa Chiveve mjini Beira.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk85, James Kotei, Clatous Chama/Shiza Kichuya dk80, John Bocco, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk70 na Emmanuel Okwi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAIFUMUA MBABANE SWALLOWS 4-0 MANZINI NA KUBISHA HODI HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top