• HABARI MPYA

    Sunday, December 02, 2018

    KAMA LWANDAMINA, HATA ZAHERA HATAWEZA KUMVUMILIA KAKOLANYA

    MSHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta ndiye mchezaji mkubwa zaidi Tanzania kwa sasa akiwa anachezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
    Kwa muhtasari historia ya Mbwana inaanzia Mbagala Market alipoibukia klabu ya Mbagala Market ambayo baadaye ilinunuliwa na mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji na kuwa African Lyon.
    Baada ya kung’ara katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara akiwa na klabu ya African Lyon, mwaka 2010 Mbwana Ally Samatta akasajiliwa na vigogo wa soka nchini, Simba SC.
    Lakini mzunguko wote wa kwanza wa Ligi Kuu wakati huo ikidhaminiwa na kampuni ya Vodacom, Samatta hakucheza kwa sababu alisusa kwa kuwa hakutimizwa ahadi alizopewa wakati anasajiliwa.
    Watu wa karibu yake waliposikia habari hizo wakamfuata na kumshauri arejee kazini akacheze, akusanye uzoefu na kukuza uwezo wake, maslahi bora yatakuja baadaye.
    Katika msimu wake wa kwanza tu baada ya kuonyesha uwezo wake akasajiliwa na klabu TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako alikwenda kufanya vyema mno na kukuza uwezo wake maradufu.
    Samatta alishinda mataji yote makubwa akiwa na Mazembe, likiwemo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika akaenda kucheza hadi Klabu Bingwa ya Dunia mara mbili na akashinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika baada ya kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo mikubwa zaidi ya klabu barani.
    Haikuwa ajabu baada ya mafanikio hayo Samatta akahamishia maisha yake ya soka Ulaya akichezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambako pamoja na kwamba haijawahi kuwekwa wazi analipwaje, lakini si chini ya dola za Kimarekani 20,000 kwa mwezi.  
    Nimekumbuka hadithi ya Samatta kwa sababu ya mlinda mlango Beno David Kakolanya, ambaye yupo katika msimu wa tatu tangu asajiliwe Yanga SC akitokea Tanzania Prisons ya Mbeya.
    Kwa muda wote huo Beno David Kakolanya amedaka mechi 24 tu, wakati chipukizi, Ramadhani Awam Kabwili aliyesajiliwa Januari mwaka huu kama kipa wa tatu na wa kikosi cha vijana, tayari amedaka mechi 19 za kikosi cha kwanza.
    Kakolanya alisajiliwa kama kipa wa kwenda kuchukua nafasi za makipa walioonekana wanaelekea kuchoka, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’ mwaka juzi.
    Lakini mwaka jana wote, Dida na Barthez waliondoka na pamoja na kwamba ilikuwa nafasi nzuri kwa Kakolanya kuwa kipa wa kwanza wa Yanga, ameendelea kuwa wa kudaka kwa nadra.
    Ni kipa mwenye uwezo mkubwa na hodari, anayejituma uwanjani na ukimtathmini vizuri kwa sasa ndiye anaweza kuwa mlinda mlango mzuri zaidi.
    Lakini Beno hapana shaka anakwamisha na sababu za nje ya Uwanja kuwa kipa tegemeo siyo tu kwa klabu yake hata timu ya taifa.
    Alisajiliwa wakati wa kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye aliendelea kumtumia kipa wa baada ya Dida na Barthez, lakini hata baada ya ujio wa kocha mpya, Mzambia, George Lwandamina bado Beno hakuwa kipa wa kutumainiwa Yanga.
    Lwandamina alichoshwa na tabia zake akaamua kuagiza aondolewe moja kwa moja kikosini, lakini bahati yake baada ya kuondoka kwa Mzambia huyo akapewa mkataba mpya.
    Hata hivyo katika miezi mitatu tu ya awali ya kocha mpya, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Beno tena amekuwa tatizo.
    Baada ya mwanzo mzuri msimu huu akiudhihirishia uma wa wapenda soka Tanzania kwamba yeye ni kipa mzuri kwa kudaka kwa uhodari mkubwa kwenye mechi kadhaa ngumu ikiwemo dhidi ya mahasimu, Simba Septemba 30, mwaka huu, ilidhaniwa Beno amebadilika.
    Lakini wiki iliyopita mchezaji huyo kwa pamoja na Nahodha na beki wa timu hiyo, Kelvin Yondan waliripotiwa kugoma kushinikiza walipwe madai yao.
    Kwa Yondan ni wa kumuacha alivyo maana katika umri wake wa utu uzima akiwa anamalizia soka yake amekwishajifunza mengi na kuzingatia ni juu yake.
    Lakini Beno ni kipa ambaye bado ana nafasi kubwa ya kuyapigania maisha yake ya kisoka ili afike mbali zaidi – hivyo kugoma kwa kutolipwa mishahara au fedha za usajili ni kujikomoa yeye mwenyewe.
    Beno anahitaji kucheza ili kuongeza uzoefu na uwezo wake afikie kuwa kipa wa kwanza wa nchi yake na kudaka mechi nyingi za kimataifa ambazo zinaweza kumfanya aonekane na klabu kubwa za nje zimchukue akanufaike kwa maslahi zaidi kutokana na kipaji chake.  
    Lakini badala yake analeta kitu kinachoitwa maringo bila kujua kwamba anajikomoa yeye mwenyewe kwa sababu badala ya kutumia muda huu kupambana kuonyesha uwezo wake aonekane na kuondoka nchi  hii, anaupoteza kwa kukaa nyumbani akisubiri alipwe fedha za usajili na malimbikizo ya mishahara ambayo wachezaji wengine wote wnadai Yanga.
    Kabwili anatumia vizuri maringo ya Kakolanya kwa kudaka kwa bidii na kuendelea kuongeza ujuzi na uzoefu, hivyo kuzidi kuweka hai ndoto zake siyo tu za kuwa kipa wa kwanza wa Yanga, bali pia kurudi timu ya taifa na siku moja akacheze Ulaya. 
    Inafahamika Yanga inakabiliwa na hali ngumu kifedha kwa sasa na wachezaji karibu wote wana madai yanayofanana, fedha za usajili na mishahara ya miezi isiyopungua mitatu – Beno anajisikiaje kugoma wakati wenzake wanaendelea kuipigania timu?  
    Ndiyo maana kocha Mzambia, George Lwandamina alimfukuza kwenye timu kwa sababu aligoma kwa sababu kama za sasa na bila shaka hata kocha mpya, Mkongo Mwinyi Zahera hataweza kumvumilia Beno – labda abadilike.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA LWANDAMINA, HATA ZAHERA HATAWEZA KUMVUMILIA KAKOLANYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top