• HABARI MPYA

    Thursday, August 02, 2018

    SIMBA SC KUMENYANA NA MABINGWA WA MOROCCO KESHO ISTANBUL, JUUKO ARUDISHWA RASMI KIKOSINI

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Simba SC kesho inatarajiwa kucheza mechi yake ya pili ya kujipima katika kambi yake ya Uturuki, itakapomenyana na mabingwa wa Morocco, Ittihad Riadi de Tanger (IRT).
    Msemaji wa klabu ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba kila kitu kimekamilika kuelekea mchezo huo na kesho watamenyana mjini Istanbul.  
    Mechi ya kwanza mabingwa hao wa Tanzania walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na MC Oujder ya Morocco pia jana jioni.
    Na huo ulikuwa mchezo wa kwanza kabisa kwa kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia Adel Zrena Kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili na Muharami Mohammed ‘Shilton’ kocha wa makipa na wa kwanza wa msimu pia.

    Kikosi cha Simba SC kilichoweka kambi katika hoteli ya Reen Park & Resorts mjini Istanbul, kikifanya mazoezi yake katika moja ya viwanja saba vilivyoizunguka hoteli hiyo, kinatarajiwa kurejea nchini Agosti 5 tayari kwa tamasha la kila mwaka la klabu, Simba Day ambalo hufanyika Agosti 8 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Na siku hiyo, Simba SC itamenyana na mabingwa mara mbili wa Afrika, Asante Kotoko ya Ghana  waliobeba taji hilo enzi za Klabu Bingwa Afrika katika miaka ya 1970 na 1983. 
    Wakati huo huo: Beki Mganda, Juuko Murshid ataendelea kuichezea Simba SC baada ya kurejea nchini kufuatia mipango ya kujiunga na SuperSport United ya Afrika Kusini kugonga mwamba.
    Juuko ni kati ya wachezaji watatu wa Simba ambao hawajasafiri na timu kwenye kambi ya Uturuki, wengine beki mzawa, Salim Mbonde ambaye ni majeruhi na kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
    Juuko aliyebakiza mwaka mmoja na ushei katika mkataba wake Simba anafanya idadi ya wachezaji tisa wa kigeni ndani ya timu hiyo, wengine wakiwa ni Mganda mwenzake, Emmanuel Okwi, Waghana Nicholas Gyan, Asante Kwasi, James Kotei, Pascal Wawa kutoka Ivory Coast, Clatus Chama kutoka Zambia, Meddie Kagere na Haruna Niyonzima Kutoka Rwanda.
    Na kulingana na kanuni mpya ya usajili wa wachezaji wa kigeni ya wachezaji 10, Simba SC ina nafasi moja zaidi ya mchezaji wa kigeni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUMENYANA NA MABINGWA WA MOROCCO KESHO ISTANBUL, JUUKO ARUDISHWA RASMI KIKOSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top