• HABARI MPYA

    Wednesday, August 08, 2018

    SALAMBA AKOSA PENALTI SIMBA SC YALAZIMISHA SARE 1-1 NA ASANTE KOTOKO UWANJA WA TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Asante Kotoko ya Ghana katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni leo.
    Ulikuwa mchezo mzuri uliotanguliwa na shamrashamra za tamasha la Simba Day kwa burudani mbalimbali zikiwemo za muziki kutoka kwa wasanii tofauti, ambalo lilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kama mgeni rasmi.  
    Simba SC walio chini ya kocha Mbelgiji, Patrick J Aussems waliuanza vizuri mchezo huo wakisukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Kotoko, lakini safu ya ulinzi ya timu ya Ghana ilikuwa imara mno.
    Washambuliaji wa Simba, Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere na Mganda Emmanuel Okwi walicheza kwa uelewano mkubwa na kutengenezeana nafasi kadhaa, lakini kipa wa Kotoko, Felix Annan aliokoa kwa ustadi mkubwa.
    Adam Salamba (kulia) akisikitika baada ya kukosa penalti leo 
    Emmanuel Okwi (kushoto) akifumua shuti katika mchezo wa leo
    Cletus Chama akitoa pasi baada ya kuwatoka wachezaji wa Asante Kotoko 

    Meddie Kagere akiudhibiti mpira dhidi ya beki wa Asante Kotoko, Agyman Badu

    Kwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza Kotoko walikuwa wana kazi ya kuzuia mashambulizi ya Simba SC kabla ya kibao kugeuka ghafla mwishoni mwa kipindi hicho na kupata bao la kuongoza kwa shambulizi la kushitukiza. 
    Bao hilo lilifungwa na mshabuliaji, Obeid Owusu dakika ya 44 aliyemalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti kali la Songne Yocouba aliyemhadaa beki mkongwe, Erasto Nyoni.
    Kipindi cha pili Simba SC walirudi na maarifa mapya, wakicheza kwa kuzuia vizuri na kushambulia kwa kasi, lakini ikawachukua muda hadi dakika 15 za mwisho kusawazisha. 
    Alikuwa ni mshambuliaji kipenzi cha wapenzi wa Simba SC, Emmanuel Okwi aliyefunga bao hilo dakika ya 76 akimalizia krosi nzuri ya winga Shiza Ramadhani Kichuya.
    Simba ikapoteza nafasi ya kupata bao la ushindi baada ya mshambuliaji wake, Adam Salamba kumdakisha penalti kipa Felix Annan dakika ya 85, kufuatia yeye mwenyewe kuchezewa rafu na beki wa Kotoko, Amos Frimpong.
    Baada ya hapo timu timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu hadi filimbi ya mwisho ya refa Hance Mabena wa Tanga kuhitimisha mchezo huo.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe/ Nicholas Gyan dk29, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas mkude, James Kotei/Hassan Dilunga dk57, Cletus Chama, Meddie Kagere/Adam Salamba dk46, Emmanuel Okwi na Shiza kichuya.
    Asante Kotoko; Felix Annan, Amos Frimpong, Augustine Sefah, Agyman Badu, Wahad Adams, Douglas Awusu, Jordan Apoku, Prince Afquah, Michael Yobboah, Songne Yocouba/Appia Kubi Samuel dk76 na Ibrahim Osman/Obed Owusu dk30.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SALAMBA AKOSA PENALTI SIMBA SC YALAZIMISHA SARE 1-1 NA ASANTE KOTOKO UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top