• HABARI MPYA

    Thursday, August 09, 2018

    RAIS DK MAGUFULI, MSTAAFU DK KIKWETE WAUAGA MWILI WA MSANII KING MAJUTO LEO DAR

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete wameshiriki zoezi la kuuaga mwili wa msanii wa vichekesho marehemu Amri Athumani ‘King Majuto’ katika ukumbi wa Karimjee mjini Dar es Salaam. 
    Ibada ya kuusalia mwili wa marehemu King Majuto imeongozwa na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakari Zubeiry ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam. 
    Marehemu King Majuto ameagwa leo na kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao mkoani Tanga kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho nyumbani kwake, Tanga.
    King Majuto amefariki dunia Saa 1:30 usiku wa jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili mjini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa matibabu kufuatia hali yake kubadilika na kuwa mbaya wiki iliyopita.
    Dk. John Pombe Magufuli akisoma dua zake mbele ya mwili wa msanii wa vichekesho, marehemu Amri Athumani ‘King Majuto’ leo ukumbi wa Karimjee mjini Dar es Salaam. 

    Rais Dk. John Pombe Magufuli akiwa na Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete huku Mufti Abubakar Zubeiry akiongoza ibada ya kuusalia mwili wa marehemu King Majuto 

    King Majuto alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka jana na Mei 4 mwaka huu akapelekwa India kwa matibabu kabla ya kurejea Juni 22 mwaka huu na kutangaza rasmi kustaagu shughuli zote za sanaa kwa sababu za Kiafya.
    Alirejea anasukumwa kwenye kiti maalum kuashiria kwamba pamoja na matibabu yake nje ya nchi, bado afya haikuwa njema sana. 
    Na wiki iliyopita alikimbizwa tena katika hospitali ya Muhimbili baada ya hali kubadilika ghafla na kuwa mbaya tena, ambako alilazwa ICU kabla ya usiku wa jana kuaga dunia.
    King Majuto Alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule ya Msambwini mkoani humo na hadi anafariki amecheza zaidi ya filamu 1,000.
    Hizo ni pamoja na; Lolita, Sio Sawa, Mama Ntilie, Nahama,Gumzo, Mrithi Wangu, Rent House, Ndoa ya Utata, Daladala, Nimekuchoka, Mbegu, Zebra, Shikamoo Mzee, Tabia, Utani, Tikisa, Trouble Maker, Gundu, Kizungunguzu, Shoe Shine, Street Girl, Faithful, Mtego wa Panya, Boss, Back with Tears, Sikukuu ya Wajinga, Nyumba Nne, Chips Kuku, Kitu Bomba, Ndoto ya Tamaa, Lakuchumpa, ATM, Bishoo, Tupo Wangapi, Moto Bati, Varangati, Out Side, Pusi na Paku, Juu kwa Juu, Swagger, Oh Mama, Jazba, Mke wa Mtu Sumu, Mbugila, Kidumu, Mkali Mo, Mpela Mpela, Utanibeba, Babatan, Mjomba, Msela wa Manzese, Karaha, Mpango Sio Matumizi, Mume Bwege, Shuga Mammy, Embe Dodo, Nakwenda Kwa Mwanangu, Seaman, Naja Leo Naondoka Leo Tanga, Mgeni Njoo, Kuwadi, Kulipa Tabu, Uso wa Mbuzi, Machimbo, Fundi Feni, Mwizi wa Kuku, Mtu Mzima Hovyo, Wake Up, Vituko Show Vol. 10, Bettery Low, Brothers, Alosto, Back from New York, Kipofu, Koziman Vol 21, After Money, Talaka Yangu, Gereji, Welcome Back, Mshamba, Pedeshee, Waiter, Inye Plus, Inye Gwedegwede na Inye Vol.1.
    Inasemekana King Majuto ndiye muigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza huku akifanya kazi na shirika la filamu Tanzania (Tanzania Film Company-TFC). 
    Alianza kuigiza mwaka 1958 akiwa na umri wa miaka tisa kuanzia shuleni kabla ya kujiunga na DDC kibisa mwaka 1983 ambacho ndicho kilimpatia umaarufu mkubwa. 
    Baadaye alijiunga na Muungano Culture Troupe chini ya Dk, Norbet Chenga, Tanzania One Theatre (TOT) chini ya Kapteni John Komba (marehemu) kabla ya kuamua kufanya zake binafsi.  King Majuto atabaki kuwa msanii mkubwa kwenye historia ya sanaa za filamu na uchekeshaji Tanzania. Buriani Mzee Majuto. Umeyamaliza yako ya duniani. Nenda kwa mola wako. Na Mola akupumzishe kwa amani. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS DK MAGUFULI, MSTAAFU DK KIKWETE WAUAGA MWILI WA MSANII KING MAJUTO LEO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top