• HABARI MPYA

  Friday, August 03, 2018

  KWA NINI TIMU YA WANAWAKE HAITHAMINIWI PAMOJA NA KUPEPERUSHA VYEMA BENDERA YA TANZANIA KIMATAIFA?

  Na Ibrahim Jeremiah, DAR ES SALAAM
  TIMU ya soka ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens, Julai 27, mwaka huu ilitwaa Ubingwa wa Kombe la Kombe la CECAFA Challenge kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Ethiopia Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda.
  Pamoja na ushindi huo wa rekodi na kihistoria, lakini Kilimanjaro Queens walirejea nyumbani kwa basi, jambo ambalo limewasikitisha wapenzi wengi wa soka wakiona mabinti hao hawajapewa thamani inastahili.
  Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakiongozwa na Rais, Wallace Karia wamepanda ndege kurejea Dar es Salaam kifahari, wakati wachezaji waliopigania heshima ya nchi wakisota barabarani kwa zaidi ya Kilomita 1500 kurudi nyumbani na Kombe lao kwa basi.
  Nyota wa Kilimanjaro Queens, Fatuma Issa 'Fetty Densa' ambaye alikuwa Mchezaji Bora wa Mashindano

  Ushindi huo uliifanya Kilimanjaro Queens kumaliza na pointi saba sawa na Uganda, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa moja lakini wastani wao mzuri wa mabao unawapa taji la pili mfululizo la CECAFA Challenge. 
  Siku hiyo Ethiopia ilitangulia kwa bao la Meseru Abera dakika ya 29 kabla ya Tanzania kuzinduka kipindi cha pili na kuwafanyia ‘ubaya’ mabinti wa Kihabeshi kwa mabao ya Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ dakika ya 46, Donisia Daniel dakika ya 56, Stumai Abdallah dakika ya 61 na Fatuma Mustafa dakika ya 89.
  Ethiopia ilimaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake sita, wakati Kenya ilikuwa ya nne kwa pointi zake nne sawa na wenyeji, Rwanda walioshika mkia.
  Pamoja na kuburuza mkia, lakini Rwanda ndiyo timu pekee iliyowafunga mabingwa Tanzania Bara, 1-0 katika mchezo wa kwanza kabisa.
  Kilimanjaro Queens wakiwa chini ya kocha Bakari Shime, aliyekuwa anasaidiwa na Edna Lema wanafanikiwa kutetea taji walilolibeba mwaka 2016.
  Mwaka 2016 michuano hiyo ilifanyika kwa mtindo wa makundi, baadaye mtoano kuanzia Nusu Fainali wakati mwaka huu mashindano yamechezwa kwa mtindo wa Ligi, na bingwa ameamuliwa kwa pointi nyingi. 
  Pamoja na mafanikio hayo, lakini cha ajabu habari hii kubwa ya kulitangaza Taifa na ya kutangaza ushujaa wa Watanzania hawa Wanawake haijapewa uzito unaostahili.
  Timu ya Taifa ya Wanaume imekuwa ikituangusha na kutukatisha tamaa kila siku, lakini hawa wamekuwa wakitupa faraja mara nyingi sana
  Nafikiri wanahitaji kupewa heshima ya kipekee na Taifa litambue kuwa kuna wawakilishi wameipeperusha Bendera yetu vizuri
  Tunazungumzia Usawa; Sasa hivi mpaka tuna makamu wa Rais Mwanamke, Mama Samiah Suluhu lakini bado tunawasahau Wanawake wa chini.
  Naomba Viongozi wa Michezo kuanzia Wizarani mtafute platform ya kuwapa pongezi hawa mashujaa wa Taifa letu
  Wafikishwe Bungeni kama zinavyofikishwa timu nyingine, wapewe heshima zote na ikiwezekana wafikishwe  Ikulu wakamkabidhi baba yao Kombe
  Wamwambie Bendera uliyotukabidhi tuipeperushe tumeipeperusha vema na tumekuletea ulichotutuma tukakichukue.
  Kwa kufanya hivi tutakuwa tumemthamini Mwanamke lakini pia tutakuwa tumewapa ari ya kujihusisha na kujibidiisha na Michezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KWA NINI TIMU YA WANAWAKE HAITHAMINIWI PAMOJA NA KUPEPERUSHA VYEMA BENDERA YA TANZANIA KIMATAIFA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top