• HABARI MPYA

  Sunday, May 15, 2016

  VIONGOZI WALIKUWA ZAMANI, SIKU HIZI MAJANGA TU

  KIHISTORIA udhamini katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ulikuja kwa mara ya kwanza mwaka 1996, wakati Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ilipoleta ahueni hiyo kupitia bia ya Safari Lager.
  Lakini Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilianza kuchezwa mwaka 1965 na tangu wakati huo tuna orodha ndefu ya mabingwa kuanzia Cosmopolitan na hawa sasa Yanga SC na historia nzuri ya mashindano.
  Bila ya udhamini, timu zote za Ligi Kuu ziliweza kufika vituoni na kucheza mechi zao.
  Na huo ni wakati ambao miundombinu ya nchi hii ilikuwa mibovu kwa maana ya barababara zilikuwa mbovu, timu zilisafiri kwa muda mrefu kutoka umbali mdogo wa safari.
  Hakukuwa na wadhamini, lakini timu hazikukosa vifaa vya mazoezi wala kutumia katika mechi. Hakukuwa na ruzuku yoyote zaidi ya makato.

  Timu zetu hazikuweza kukwama hata kucheza michuano ya Afrika au ile ya Afrika Mashariki na Kati – japokuwa hazikuwa na udhamini.
  Kulikuwa kuna timu za taasisi na mashirika, lakini tulikuwa tuna timu za uraiani zikiwemo zile kongwe Simba na Yanga African Sports, Coastal Union, Nyota Nyekundu, Cosomo, ambazo zilimudu kushiriki kikamilifu Ligi Kuu.
  Nje ya Uwanja, tulishuhudia mafanikio ya timu hizo zikiweza kusimamisha majengo mazuri katikati ya miji mfano Simba SC pale Msimbazi na Yanga SC pale Jangwani na Mtaa wa Mafia.
  Zilikuwa timu za soka kweli, zilikuwa zina timu za vijana maarufu kama Simba B au Yanga ambazo zina historia ya kutoa wachezaji waliogeuka kuwa nyota wa taifa kama Juma Pondamali kwa Yanga au Nico Njohole kwa Simba na wengineo wengi.
  Leo ni miaka 20 tangu Ligi Kuu ipate udhamini kwa mara ya kwanza – na sasa tunazungumzia neema zaidi katika ligi hiyo.
  Ina udhamini mnono zaidi ya Vodacom na pia inaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam, inayolipa mamilioni kwa klabu.
  Kwa ufupi timu za Ligi Kuu zinapata mgawo wa Vodacom na Azam TV walioanza miaka miaka mitatu iliyopita.
  Haya ni mabadiliko makubwa ambayo kwa bahati mbaya yameshindwa kubadilisha taswira ya soka yetu.
  Timu sasa hazinunui vifaa, kwa sababu vinatoka kwa wadhamini na bado kuna timu mbali na wadhamini wa Ligi Kuu zina wadhamini binafasi, mfano Simba na Yanga zinadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro.
  Viongozi wa zamani wa Simba na Yanga waliweza kuziendesha timu hizi bila udhamini, lakini zilikuwa zina timu za vijana na zilishiriki mashindano kikamilifu ndani na nje ya nchi.
  Inafahamika wazi msingi wa kuzalisha wachezaji bora wa baadaye ni kuwa na timu bora za vijana na ndiyo maana katika kanuni za Ligi Kuu hivi sasa, kila timu inayoshiriki ligi hiyo inapaswa kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
  Agizo hilo kwa timu yenye viongozi wenye fikra pevu zinaweza kutengeneza msingi wake zenyewe wa kuzalisha vijana kwa kuunda timu za vijana kuanzia chini ya umri hata wa miaka 12.
  Ajabu pamoja na timu za Ligi Kuu kushinikizwa kuwa na timu za vijana, lakini zimekuwa hazichezi mashindano yoyote.
  TFF imeshindwa kuendesha ligi ya vijana na ukiuliza sababu haswa hakuna.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi anapaswa kutambua kwamba Said El Maamry alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) na akaendesha Ligi Kuu bila fungu lolote la udhamini, zaidi ya makato.
  Leo Ligi Kuu ina wadhamini wawili Vodacom na Azam TV, TFF inashindwaje kuwa na Ligi ya vijana?
  Viongozi wa Simba na Yanga wa sasa wanapaswa kujua kwamba, viongozi wa zamani wa klabu hizo waliziongoza bila udhamini na zikaweza kushiriki mashindano kikamilifu.
  Kana kwamba hiyo haitoshi, majengo hayo ya sasa ya Simba na Yanga yaliachwa na viongozi hao wa zamani miaka ya 1970.
  Leo tuna viongozi wanaoitwa wasomi na wa kisasa, lakini wameshindwa kuleta mapya katika klabu hizo na mbaya zaidi wanashindwa hata kuziongoza kushiriki mashindano kikamilifu.
  Wanashindwa kuwa na timu za vijana – wanashindwa kuwalea vizuri wachezaji wao kila siku ni migogoro nao tu. Ndiyo maana huwa inafikia wakati tunasema, viongozi walikuwa zamani, siku hizi majanga tu! 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VIONGOZI WALIKUWA ZAMANI, SIKU HIZI MAJANGA TU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top