• HABARI MPYA

  Thursday, May 19, 2016

  ULIMWENGU ‘AWATAMANI’ YANGA, ASEMA SASA WAMEKUWA TIMU KWELI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema anatamani wapangwe kundi moja na timu ya nyumbani kwao, Tanzania, Yanga SC katika Kombe la Shirikisho Afrika.
  Yanga na Mazembe zote zimefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuwatoa wapinzani wao juzi na jana.
  Mazembe walianza kufuzu juzi kwa faida ya bao le ugenini, baada ya sare ya jumla ya 2-2 dhidi ya Stade Gabesien ya Tunisia ikishinda 1-0 nyumbani Lubumbashi wiki iliyopita kabla ya juzi kufungwa 2-1 Tunisia.
  Thomas Ulimwengu anatamani Mazembe wapangwe kundi moja na Yanga

  Yanga ikafuatia kufuzu jana kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola baada ya kufungwa 1-0 mjini Dundo ikitoka kushinda 2-0 wiki iliyopita Dar ea Salaam.
  Na Ulimwengu amesema; “Nawapongeza sana Yanga kwa kufuzu, hayo ni matunda ya uwekezaji katika timu yao, mpira unahitaji kuwekeza fedha, Yanga wameweka fedha, nawapongeza sana, sasa imekuwa timu ya ushindani,”.
  Aidha, Ulimwengu amesema anatamani katika droo ya CAF wapangwe na Yanga na atafurahi kucheza dhidi ya timu ya nyumbani. “Itakuwa mechi nzuri sana sisi na Yanga, yaani mimi nacheza pale Taifa dhidi ya Yanga, tamu sana,”amesema Uli maarufu kwa jina la Rambo mjini Lubumbashi.
  Mbali na Yanga na Mazembe, timu nyingine zilizofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ni FUS Rabat, Kawkab Marrakech zote za Morocco, Etoil du Sahel ya Tunisia, Ahli Tripoli ya Libya, MO Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.
  FUS Rabat imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 4-0, ikishinda 4-0 nyumbani dhidi ya Stade Malien ya Mali baada ya sare ya 0-0 ugenini.
  Kawkab Marrakech imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya El Merreikh ya Sudan, ikishinda 2-0 nyumbani baada ya kufungwa 1-0 ugenini.
  Ahli Tripoli imefuzu kwa bao la ugenini dhidi ya Misr Makkassa ya Misri, ikilazimisha sare ya 1-1 ugenini baada ya sare ya 0-0 nyumbani.
  Medeama imefuzu kwa bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ikishinda 2-0 nyumbani baada ya kufungwa 3-1  ugenini.
  Etoile du Sahel imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya C.F. Mounana ya Gabon ikifungwa 1-0 ugenini baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani.
  Droo ya makundi yote, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho inatarajiwa kupangwa Jumanne ya Mei 24, 2016 makao makuu ya CAF, Cairo nchini Misri saa 6:30 mchana.
  Timu zilizofuzu Ligi ya Mabingwa ni Enyimba ya Nigeria, Al Ahly na Zamalek za Misri, AS Vita ya DRC, Asec Mimosas ya Ivory Coast, Wydad Casablanca ya Morocco, ES Setif ya Algeria na Zesco United ya Zambia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU ‘AWATAMANI’ YANGA, ASEMA SASA WAMEKUWA TIMU KWELI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top