• HABARI MPYA

    Sunday, May 15, 2016

    SERENGETI BOYS YAWATOA JASHO WAMAREKANI INDIA, SARE 1-1

    Na Mwandishi Wetu, GOA
    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania, Serengeti Boys imetoa ya sare kufungana bao 1-1 na Marekani katika mchezo wake wa kwanza wa michuano ya kirafiki ya vijana Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa, India leo.
    Michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka India (AIFF) ili kuipa mazoezi timu yake, ikishirikisha timu mbalimbali duniani, mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza.
    Jean Julien alianza kuifungia Marekani dakika ya tano tu, lakini Mohamed Abdallah akaisawazishia Serengeti Boys dakika ya 19.
    Wachezaji wa Serengeti Boys na Marekani kabla ya mechi ya leo

    Serengeti itashuka tena dimbani Mei 19 kumenyana na Korea Kusini kuanzia Saa 7:30 mchana kwa saa za India.
    Kikosi hicho cha wachezaji 22 cha Serengeti chini ya Kocha Bakari Shime kipo mjini humo kwa ajili ya mashindano hayo, yatakayofikia tamati Mei 25, mwaka huu.
    Kikosi hicho ni makipa; Ramadhan Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio wakati mabeki wa pembeni ni Kibwana Shomari, Nicson Kibabage, Israel Mwenda na Ally Msengi.
    Mabeki wa kati ni Issa Makamba, Nickson Job na Ally Ng'anzi huku viungo wakiwa ni Maulid Lembe, Asad Juma, Kelvin Naftari, Yasin Mohamed na Syprian Mwetesigwa na washambuliaji ni Aman Maziku, Rashid Chambo, Enrick Nkosi, Yohana Mkomola, Mohamed Abdallah, Shaban Ada na Muhsin Mkame.
    Maofisa walio na timu huko ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ayoub Nyenzi, Mshauri wa ufundi wa timu za vijana, Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime, Kocha wa Makipa Mohamed Muharami, Daktari wa timu, Shecky Mngazija na mtunza vifaa, Edward Edward.
    Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.
    AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAWATOA JASHO WAMAREKANI INDIA, SARE 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top