• HABARI MPYA

    Monday, May 09, 2016

    JULIO AWAPASHA SIMBA NA YANGA; “HESHIMUNI MAKOCHA WAZAWA, WANAWEZA KULIKO WAGENI”

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Mwadui FC, Jamhuri Mussa Kihwelo ameziasa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga kuheshimu makocha wazawa na kuacha kupapatikia makocha wa kigeni.
    Julio ameyasema hayo jana baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mwadui FC ikiilaza Simba SC 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la kiungo Jamal Mnyate.
    Na baada ya ushindi huo, Julio akakumbushia alivyoondolewa kwa dharau Simba miaka mitatu iliyopita pamoja na aliyekuwa Kocha wake Mkuu, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King KIbadeni’.
    Jamhuri Kihwelo akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo wa jana. Kulia ni Kombe bandia la ubingwa wa Ligi Kuu alilowekewa na mashabiki wa Yanga

    “Leo nimedhihirisha mimi ni kocha bora kwa kuifunga Simba, hizi ni salamu tosha kwa viongozi wa Simba ambao walinifukuza mimi na Kibadeni wakaleta makocha Wazungu na hadi leo timu haijafanya chochote,”alisema Julio.
    Beki huyo wa zamani wa kimataifa nchini aliyewika Simba SC miaka ya 1990, amesema yeye na Kibadeni waliondolewa kimizengwe na kufanya vibaya kwa timu hiyo hivi ni laana yao.
    “Sisi tuliondolewa kimizengwe, timu ilikuwa inafanya vizuri haijapoteza mechi, wakaja watu wakasema tuondoke, sasa hii ni laana yetu mimi na Kibadeni,”alisema Julio.
    Lakini Julio kwa ujumla amezitaka klabu za Simba na Yanga kuheshimu makocha wa kigeni kwa sababu wana uwezo mkubwa na sasa pia wana vyeti vya kiwango cha juu, vinavyowawezesha kufundisha popote.
    Julio akatolea mfano kocha mzalendo Charles Boniface Mkwasa anavyoendelea vizuri katika timu ya taifa, Taifa Stars tangu arithi mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij.
    “Mkwasa yule pale amepewa timu ya taifa, mambo kidogo mazuri sasa hivi, lakini alipokuwa Mzungu ilikuwa hovyo,”alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JULIO AWAPASHA SIMBA NA YANGA; “HESHIMUNI MAKOCHA WAZAWA, WANAWEZA KULIKO WAGENI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top