• HABARI MPYA

  Monday, May 16, 2016

  NANI KAMA MZEE YUSSUF, KHADIJA KOPA NA ISHA MASHAUZI?

  INAWEZEKANA kabisa kuwa kuna wasanii wengi wazuri, lakini wenye nyota zao wakawa wachache – hiyo ni tunu ya Mwenyezi mungu.
  Lakini pia kunaweza kuwa na wasanii wengi wengi mahiri lakini mwenye mvuto wa kibiashara wakawa wa kutafuta kwa toshi – hili nalo  ndio lile watoto wa mjini wanasema ‘tatizo nyota’.
  Naomba niwazungumzie watu watatu wanaokimbiza katika muziki wa taarab – Mzee Yussuf, Khadija Kopa na Isha Mashauzi ambao hakuna ubishi kuwa kwa sasa unapozungumzia biashara ya taarab kwa mlengo wa kimafanikio basi laziwa uvitaje vichwa hivi vitatu kabla hujaendelea kutaja majina mengine. 

  Kabla ya yote napenda niwaombe radhi wale wote ambao ntakuwa sijawasifu au kuwataja kwenye makala hii maana wakati mwingine huwa inaumiza kidogo pale sifa zilizotukuka zinapokupitia mkono wa kushoto.
  Bila kujali mwimbaji au mpiga vyombo, Mzee Yussuf, Khadija Kopa na Isha Mashauzi ndio wasanii wa taarab wenye mashabiki wengi zaidi, ndio ambao kazi zao zinazungumziwa zaidi, ndio ambao uwepo wao kwenye majukwaa ya taarab huteka zaidi hisia za watu.
  Jambo hilo si la leo wala jana, ni la zaidi ya juzi. Unawezaje kumkataa Khadija Kopa ambaye amekuwa akitamba miaka na miaka, amekuwa supastaa tangu mwaka 1992 alipotua Dar es Salaam kulitumikia kundi la TOT.
  Lakini hata hao TOT hawakumtoa vichochoroni, walimtoa Zanzibar kwenye kundi la Culture akiwa tayari anasumbua kwa kwenda mbele na nyimbo zake kali ukiwemo “Kadandie”.
  Tangu kipindi hicho Khadija Kopa hajashuka kisanii wala kibiashara – wako wasanii wengi wa rika lake, aliofanya nao kazi tangu miaka hiyo ya 90 ambao kwa sasa kama hawajafilisika kisanii basi wamefilisika kibiashara au vyote viwili.
  Mzee Yussuf, huyu naweza kumwita mwana mageuzi ambaye amekuja kuufanya muziki wa taarab upendwe na kila rika na kila jinsia.
  Wala hawajakosea walioamua kumwita Mfalme, hakika Mzee Yussuf ni fundi mwenye sauti ya aina yake, anayejua kulimiki jukwaa, anayejua aina ipi ya tungo itawashika watu. Ubora wa Mzee Yussuf unajitosheleza bila hata kuhangaika kuutaja msururu wa wasanii aliowatoa kisanii.
  Kuna mtu mmoja niliwahi kukaa naye jirani katika moja ya maonyesho ya Jahazi wakati Mzee Yussuf akiwa jukwaani akiongea maneno mawili matatu juu ya bendi yake, wala hakuimba siku hiyo. Yule bwana akaniambia kitu flani.
  Bwana yule akasema: “pamoja na kwamba leo Mzee Yussuf hajaimba, lakini nimeridhika sana kwa pale nilipomuona tu jukwaani akiongea, nimetosheka na hakika pesa yangu imeenda kihalali, nampenda Mzee Yussuf hata kwa kumuona kwenye matangazo ya biashara ya kwenye TV achilia mbali kumuona akiimba.” Naam hiyo ndiyo ile  nyota ambayo wasanii wengine wengi wanazikosa.
  Isha Mashauzi. Mwimbaji mwenye mapafu ya mbwa anayeweza kusimama jukwaani kwa masaa matatu akitupia masauti matamu huku akicheza katika namna ya itakayokufanya usichoke kumtazama.
  Aina yake ya kipekee ya uimbaji, inaitoa taarab kutoka kwenye hatua moja hadi nyingine, ni mtu anayebadika kama kinyonga, mtu ambaye akisimama tu jukwaani tayari mashabiki wanapata kiwewe, ubora wake haujalishi nani mtunzi wake, nani anayempigia chombo.
  Mzee Yussuf, Khadija Kopa na Isha Mashauzi nawapa pongezi kwa kazi nzuri, kwa kulisongesha gurudumu la taarab, lakini kaeni mkijua kuwa zipo adha nyingi za kuwa juu, zikiwemo kuchukiwa na washindani wenu, kuombewa mabaya na washindani wenu, kufanyiwa majungu na washindani wenu na zingine kadha wa kadha lakini hizo zichukulieni kama moja ya dalili za mtu kuwa STAA, wala hali hiyo isiwasumbue, pigeni kazi. WANAO WACHUKIA NI WACHACHE, WANAOWAPENDA NI WENGI.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NANI KAMA MZEE YUSSUF, KHADIJA KOPA NA ISHA MASHAUZI? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top