• HABARI MPYA

    Friday, December 14, 2018

    NDOTO ZA HARUNA MOSHI 'BOBAN' KUCHEZA YANGA ZIMETIMIA 'UZEENI'

    Na Mohammed Bhinda, DAR ES SALAAM 
    "KWANZA kabisa ningependa nikujulishe ndugu msomaji, kuwa mie niandikae ujumbe huu naitwa Mohamed Bhinda, naweza kusema kuwa ni mtu pekee niliyewahi kuiongoza klabu ya Yanga kwa takriban miaka zaidi ya ishirini kwa nyakati tofauti na nyadhifa tofauti,".
    "Sina lengo la kujisifu juu ya jina langu ndani ya klabu ya Yanga, bali nakudondolea kidogi tu ili kukuandaa msomaji juu ya nimjuavyo Haruna Moshi 'Boban',".
    "Haruna Moshi ni mmoja ya watoto wa Mzee Moshi, ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa Shirika la Reli nchini,  mzee huyo mwenyeji wa Tabora alikuwa ni mkaguzi wa tiketi ndani ya treni za shirika hilo 'TT',".
    "Familia ya Mzee Moshi imejaaliwa kuwa na vipaji vya uchezaji wa soka, licha ya watoto wake wengine, hapa tunamchukua Iddi Moshi 'Mnyamwezi' ambaye alikuwa mchezaji maarufu wa timu ya Yanga kwenye simulizi hii fupi,".

    Haruna Moshi Shaaban 'Boban' amesaini mkataba wa miezi sita kujiunga na Yanga SC

    "Mwaka 1999 mie nikiwa Meneja mkuu wa Timu ya Yanga, tulitwaa kombe la ubingwa wa Afrika Mashariki na kati nchini Uganda, wakati huo kocha mkuu alikuwa mkongo Roul Piere Shungu,".
    Mara baada ya kupata ubingwa huo, ambapo Idd Moshi alikuwa ni mmoja wa wachezaji wa Yanga, timu yetu ilipata mialiko mikoa kadhaa katika kusheherekea ubingwa huo,
    moja ya mkoa tulioalikwa ulikuwa ni Morogoro kucheza na Mtibwa mchezo wa kirafiki,"
    "Kwenye kikosi kilichokwenda mjini Morogoro, Haruna Moshi Boban naye alikuwemo, wakati huo bado mdogo sana kiumri. Kwenye mechi hiyo dhidi ya Mtibwa, Kocha Roul Shungu alimuingiza Haruna zikiwa zimebakia dakika ishirini hivi,".
    "Siku hiyo Haruna alicheza soka ya hali ya juu licha ya udogo wake, baada ya mechi kwisha kocha Shungu alishauri tumsajili, tulishauriana ni kwa namna gani tutamsajili Haruna wakati akiwa chini ya miaka 15?".
    "Wakati huo Haruna alidhamiria kuchezea Yanga, binafsi naweza kusema ndio ilikuwa ndoto yake,  wakati sisi Yanga tukisuasua juu ya umri wake, ndipo walipotokea watu wa Simba na kumpeleka Coastal Union ya Tanga na baadaye kumsajili Simba, naweza kukiri kuwa Yanga tulizembea,".
    "Miaka ikapita, ndoto za Haruna kuchezea Yanga zikawa kichwani mwake, ndipo siku aliyotaka kusaini Yanga kutoka Simba, palifanyika umafia wa kumtorosha kwenye uwanja wa Muhimbili ambapo mie nilipanga na Imani Madega kwenda kumsainisha mkataba. Nakumbuka watu wa Simba walivamia pale shule ya msingi Muhimbili na kuzima taa za uwanjani na kumteka Haruna,".
    "Tulimuandalia safari Haruna kwenda Uarabuni kwa mkataba wa mwaka mmoja, na lengo akirudi asajili Yanga, aliporudi aliikuta Yanga ipo kwenye migogoro, hivyo ilishindikana kumsimamia usajili wake,".
    "Miaka imepita na Haruna kalinda kipaji chake, leo kocha wa Yanga Mwinyi Zahera katangaza mwenyewe kuwa amemtaka Haruna Moshi 'Boban'. Ha ha haaaa, ndoto za Haruna kuchezea Yanga zimetimia, japo kwenye utu uzima,  waswahili wanasema, mwenye kujua anajua tu, kipaji hakijifichi,".
    "Karibu Haruna Moshi Shaaban, au Boban kwenye timu uliyoidhamiria kuichezea tangu utotoni, Young Africans Sports Club. Karibu Jangwani,". 
    (Makala hii imeandikwa na Mohammed Bhinda, Meneja wa zamani wa Yanga aliyewahi pia kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NDOTO ZA HARUNA MOSHI 'BOBAN' KUCHEZA YANGA ZIMETIMIA 'UZEENI' Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top