• HABARI MPYA

    Wednesday, August 08, 2018

    KARIA: BADO TUNAENDELEA NA MAZUNGUMZO NA VODACOM WAENDELEE KUDHAMINI LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM 
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba bado wapo kwenye mazungumzo na kampuni ya Vodacom juu ya mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kwenye mahojiano maalum mjini Dar es Salaam, Karia amesema kwamba anashangazwa na wanaosema kuanzia msimu ujao Ligi Kuu haitakuwa na mdhamini mkuu.
    “Inafahamika kila mkataba wa Vodacom unapofikia tamati mazungumzo huwa mazito na ya mvutano hadi makubaliano yanafikiwa dakika za mwisho kabla ya Ligi Kuu kuanza, watu wavute subira, bado tunaendelea na mazungumzo,”amesema Karia. 
    Pamoja na hayo, Karia amesema kwamba kuna uwezekano Ligi Kuu ikawa na wadhamini zaidi ya wawili msimu huu, kwani mazungumzo yanaendelea vizuri na makampuni mbalimbali.

    Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) amesema bado wapo kwenye mazungumzo na Vodacom waendelee kudhamini Ligi Kuu

    Ligi Kuu msimu wa 2018-2019 inatarajiwa kuanza Agosti 22 na hadi sasa ni Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) tu wamesaini mkataba mpya wenye thamani ya Shilingi Milioni 420 huku wasiwasi ukiwa ni juu ya wadhamini wakuu, Vodacom.
    Ligi Kuu itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya washindi wa Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC), Mtibwa Sugar ambao utafanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Agosti 18.
    Mahasimu wa jadi, Simba na Yanga watakutana Septemba 30, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi za ufunguzi za Ligi Kuu zitachezwa Agosti 22 kati ya Ruvu Shooting na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Alliance na Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Coastal Union na Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
    Mechi nyingine ni kati ya Singida United na Biashara United Uwanja wa Namfua, Singida, Kagera Sugar na Mwadui FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba zote Saa 10:00 jioni na Simba SC na Tanzania Prisons Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
    Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu utakamilishwa Agosti 23 kwa mechi kati ya JKT Ruvu na KMC Saa 8:00 mchana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Stand United na African Lyon Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Azam FC dhidi ya Mbeya City Saa 1:00 usiku.
    Ligi Kuu itafikia tamati Mei 19, mwakani (2019) ikiwa na jumla ya mechi 380 kutoka 240 msimu uliopita baada ya ongezeko la timu nne kutoka 16 za msimu uliopita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA: BADO TUNAENDELEA NA MAZUNGUMZO NA VODACOM WAENDELEE KUDHAMINI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top