• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 30, 2016

  SIMBA YAWASILISHA RISITI ZA MISHAHARA YA KESSY BENKI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe, amesema kwamba klabu ilimtimizia haki zake zote, beki Hassan Ramadhan Kessy katika kipindi chake cha chote kuwatumikia Wekundu hao wa Msimbazi.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo kutoka Marekani, Hans Poppe amesema kwamba pamoja na hayo wamewasilisha vielelezo vyote vilivyotakiwa na Kamati ikiwemo risiti za benki ya CRDB za kumuingizia mishahara yake Kessy.
  “Kessy hakuwahi kutaka kuvunja mkataba sababu ya kukosa mshahara na wakati akisaini Yanga alikuwa ndani ya mkataba na Simba… hilo halipingiki. Pamoja na hayo tumewasilisha vielelezo walivyotaka,”alisema Hans Poppe.
  Hans Poppe (kushoto) akiwa na Rais wa Simba, Evans Aveva 

  Baada ya kikao cha Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya makamu Mwenyekiti, Raymond Wawa Jumapili, Simba ilitakiwa kuwasilisha vithibitisho vya kumlipa mishahara Kessy miezi mitatu ya mwisho kuelekea kumaliza mkataba wake.
  Hiyo ilifuatia hoja iliyowasilishwa na Mwanasheria wa Yanga, Alex Mgongolwa jana katika kikao cha Kamati   
  ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji kwamba Simba haina uhalali wa madai yoyote dhidi ya Kessy kwa sababu haikumlipa mishahara kwa miezi mitatu.
  Kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Yanga walidai kwamba Simba hawakumlipa mchezaji huyo kwa miezi mitatu kuelekea mwisho wa mkataba wake na kwa mujibu wa sharia hawana haki ya madai yoyote dhidi yake.
  Na Yanga waliiomba Kamati ipokee vielelezo vya kuthibitisha kupelekwa mishahara ya Kessy kwenye akaunti yake ya benki na si vinginevyo – kwa kuwa wana wasiwasi wapinzani wao wanaweza kufoji nakala za kumlipa mkononi. 
  Simba inalalamikia klabu ya Yanga kumsajili beki Kessy akiwa hajamaliza mkataba wake Msimbazi na kwa sababu hiyo inataka kulipwa Sh. Milioni 200 ambayo ni punguzo kutoka Bilioni 1.2 walizotaka awali.
  Suala hilo lilianzia Kamati ya Maadili, ambako ilishindikana kupatiwa ufumbuzi na Kamati hiyo ikaagiza Simba na Yanga zikutane zenyewe kumalizana.
  Hata hivyo, mahasimu hao wa jadi katika soka ya Tanzania walishindwa kufikia mwafaka na wakakubaliana kumteua, Mwenyekiti wa zamani wa TFF enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania), Said El Maamry kuwasimamia katika kikao kingine cha kutafuta mwafaka.
  Bahati mbaya, Simba na Yanga mbele ya Mzee El Maamry pia wakashindwa kufikia mwafaka na suala hilo linarudishwa Kamati ya Madili.
  Viongozi wa pande zote mbili, Simba na Yanga wote watakutana mbele ya Kamati ya Maadili iliyo chini ya Mwenyekiti wake,Wakili Richard Sinamtwa kwa kikao cha kulipatia suluhisho suala hilo.
  Kamati hiyo ilisema mapema inawapa nafasi Simba na Yanga wakamalizane wenyewe na ikishindikana, suala hili litarejeshwa Kamati ya Maadili kwa uamuzi.
  Kessy alijiunga na Simba SC mwaka 2014 kutoka Mtibwa Sugar, lakini mapema tu kabla ya kumaliza mwaka wake wa kwanza aliingia kwenye mzozo na klabu hiyo akidai kutokamilishiwa yaliyomo kwenye mkataba, ikiwemo kutopewa nyumba na akagoma.
  Hata hivyo, suala hilo lilitatuliwa na mchezaji huyo akarejea kazini kabla ya kurudi kwenye matatizo tena mwishoni mwa mwaka wake wa mwisho wa mkataba.
  Simba ilimsimamsha mechi tano Kessy kwa tuhuma za kumchezea rafu isiyo ya kimchezo mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher.
  Simba ilifungwa 1-0 na Toto Jumapili ya Aprili 17, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Kessy akatolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu Edward, nyota wa zamani wa timu hiyo Msimbazi.
  Lakini mapema Februari 20, Kessy alianza kupunguza mapenzi ya wana Simba kwake, baada ya kutoa pasi fupi kumrudishia kipa Muivory Coast, Vincent Angban iliyonaswa na mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma aliyekwenda kuifungia Yanga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0.  
  Iwapo Simba SC itashindwa kuwasilisha vielelezo vya kumlipa mishahara ya miezi ya mwisho wa mkataba wake Kessy, kuna uwezekano madai yao yote yakatupiliwa mbali. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA YAWASILISHA RISITI ZA MISHAHARA YA KESSY BENKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top