• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 30, 2016

  SAMATTA AFUNGA MAWILI GENK YASHINDA 3-1 UGENINI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku huu amemaliza ukame wa mabao baada ya kufunga mara mbili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Waasland-Beveren.
  Katika mchezo huo wa Kombe la Ubelgiji uliofanyika Uwanja wa Freethiel-Stadion mjini Beveren-Waas, Samatta alifunga mfululizo bao la kwanza na la pili dakika za 15 na 43.
  Beki Mnigeria, Onyinye Wilfred Ndidi alikamilisha sherehe za mabao za Genk kwa kufunga la tatu dakika ya 80, wakati bao pekee la wenyeji lilifungwa na mshambuliaji chipukizi wa Ubelgiji, Zinho Gano.
  Baada ya muda, kwa mara ya pili mfululizo Samatta ameanza leo kama Jumamosi, siku ambayo KRC Genk ilifungwa 6-0 na KV Oostende katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.
  Samatta (kushoto) akipongezwa na wenzake usiku huu baada ya kufunga mbao mawili katika ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Waasland-Beveren

  Kabla ya hapo, Samatta alianzishiwa benchi katika mechi tatu mfululizo baada ya mara ya mwisho kuanzishwa Novemba 3 katika mechi dhidi ya Athletic Bilbao kwenye Europa League. 
  Mshambuliaji Mgiriki, Nicolous Karelis aliyekuwa anaanza mechi zilizopita mbele ya Samatta leo aliingia dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo kumpokea Nahodha wa Tanzania.
  Makali ya Samatta yalianza kupungua baada ya kuumia kwenye mchezo wa Europa League dhidi ya Rapid Wien ya Austria Septemba 15, mwaka huu Genk ikishinda 3-2 Uwanja wa Laminus Arena.
  Na siku hiyo, Samatta alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia na kutoka dakika ya 78, nafasi yake ikichukuliwa na Mbelgiji Karelis. 
  Samatta alikaa nje kwa wiki tatu na tangu hapo hata baada ya kurejea hakupata nafasi ya kuanza kutokana Karelis kufanya vizuri kabla ya kurejea mwishoni mwa wiki na leo amepangwa tena.
  Leo Samatta amecheza mechi ya 36 tangu ajiunge na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, 18 msimu uliopita na 16 msimu huu, akifunga mabao 10, matano msimu huu na matano msimu uliopita.
  Katika mechi hizo, ni 19 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na saba msimu huu, wakati 16 alitokea benchi nane msimu uliopita na 13 msimu huu – na mechi 10 hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na nne msimu huu.
  Kikosi cha W. Beveren kilikuwa: Koteles, Demir, Moors, Boljevic/Myny dk11, Writers, Michel Seck, Schwartz/Gano dk75 Ampomah/Marquet dk45 na Camacho.
  KRC Genk: Bizot, Walsh, Colley, Dewaest, Castagne, Ndidi, Pozuelo/Susic dk81 Heynen, Bailey, Samatta/Karelis dk92 na Trossard.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA MAWILI GENK YASHINDA 3-1 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top