• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 28, 2016

  SERIKALI INAZITAKIA NINI SIMBA NA YANGA?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KWA mara ya pili mfululizo wiki iliyopita, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kupitia kwa Katibu wake, Mohammed Kiganja limezuia mpango wa wafanyabiashara wanaotaka kumiliki klabu kongwe za soka nchini, Simba na Yanga.
  Kiganja alisema kuzimilikisha klabu hizo kwa watu binafsi kwa kuziondoa mikononi mwa wanachama kunaweza kuhatarisha amani.
  Tamko hilo la Kiganja lilifuatia klabu ya Simba kupanga tarehe ya Mkutano wa dharula wa mabadiliko ya katiba, ambayo ni Desemba 11 ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
  Na Simba SC iliamua kuitisha Mkutano huo, baada ya tamko la awali la BMT mwezi uliopita kuzuia michakato yote ya mabadiliko ndani ya klabu za Simba na Yanga hadi hapo mabadiliko ya Katiba yatakapofanyika.
  Lakini wakati klabu hizo zinaanza michakato ya mabadiliko ya Katiba, zengwe lingine linaibuka ambalo ni BMT kuzuia waziwazi na mpango wowote wa kuzimilikisha klabu hizo kwa watu binafsi.
  Ikumbukwe wanachama wa Simba wameafiki kumuuzia hisa asilimia 51 mfanyabiashara, Mohammed ‘Mo’ Dewji kwa Sh. Bilioni 20 wakati mahasimu wao nao, Yanga wamekubali kumkodisha klabu yao kiongozi wao mmoja kwa miaka 10.
  Bado haieleweki kama matamshi ya Kiganja ni ya kwake binafasi, au ni agizo la wakuu wake – kwa sababu amekuwa akitoa maagizo mazito katika hali ya kawaida mno. Lakini kwa kuwa hakuna kati ya viongozi wa juu wa BMT, akiwemo Mwenyekiti, Dioniz Malinzi, Kurgenzi ya Michezo na Wizara aliyemkemea au kumpinga Kiganja, tuamini huo ni msimamo rasmi wa Serikali.
  Pamoja na kuamini hivyo, tukubaliane kwamba Simba na Yanga ziliingia kwenye michakato ya mabadiliko iwe kwa shinikizo au hiari ili kujikomboa kiuchumi na pia kufuata nyayo za klabu nyingine duniani, hususan Uingereza ambazo zilibadilisha miundo yake na kumilikishwa watu.
  Hata baadhi ya nchi barani, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), klabu ya TP Mazembe imekuwa na mafanikio makubwa baada ya kumilikishwa kwa mfanyabiashara Moise Katumbi na Simba na Yanga zinatamani kufuata nyayo hizo.
  Dhahiri kiu ya wanachama wa Simba na Yanga ni kuziona klabu zao zinakuwa vizuri kiuchumi na kumudu kujiendesha kwa uhakika, ndiyo maana wanataka mabadiliko, matajiri wakabidhiwe timu waweke fedha ziwe imara zaidi na kushindania mataji makubwa Afrika na duniani.
  Lakini wakati Serikali inaona aina ya mabadiliko waliyoridhia wanachama wa klabu hizo ni hatari, ajabu haitoi mawazo mbadala ili kuzisaidia klabu hizo kujimudu kiuchumi. 
  Haitoshi Serikali kuzuia tu mabadiliko Simba na Yanga bila kutoa suluhisho mbadala la kuzisaidia klabu hizo kujikomboa kiuchumi ili zitimize ndoto za kushindana na akina TP Mazembe, Zamalek, Wydad Atletic, Setif, Mamelodi, Zesco na Esperance.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI INAZITAKIA NINI SIMBA NA YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top