• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 28, 2016

  KAKOLANYA AKAMATWA AMEPANDA BODA BODA BILA KUVAA HELMET

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA wa Yanga, Benno Kakolanya leo ameshindwa kuhudhuria mazoezi ya timu yake kufuatia kukamatwa na askari wa usalama barabarani akiwa amepanda pikipiki bila kuvaa kofia maalumu ya kujikinga kichwani, maarufu kama Helmet.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kwamba Kakolanya ni kati ya wachezaji saba ambao hawakuhudhuria mazoezi Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali.
  “Benno Kakolanya alipiga simu kutuambia amekamatwa na trafiki akiwa amepanda pikipiki bila kuvaa Helmet sasa wakati anapiga simu tena baada ya kuachiwa, tulikuwa tumekwishamaliza mazoezi, hivyo hakuja kabisa,”amesema Hafidh.
  Benno Kakolanya leo ameshindwa kuhudhuria mazoezi Yanga baada ya kukamatwa na askari wa usalama barabarani akiwa hajavaa Helmet

  Mbali na kipa huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Prisons ya Mbeya, wengine ambao hawakufika mazoezini leo ni beki Mtogo Vincent Bossou, kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, washambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, Mzambia, Obrey Chirwa na wazawa beki Hassan Kessy na mshambuliaji Malimi Busungu.
  “Bossou ana ruhusa maalum yupo kwao Togo, Ngoma ana matatizo ya kifamilia, Busungu alikuwa anashughulikia kesi yake ya ajali, Kessy naye alikuwa anashughulikia kesi yake na Simba, lakini Niyonzima na Chirwa kwa kweli sina taarifa zao,”amesema.
  Hafidh amewataja wachezaji 18 waliofika mazoezini leo kuwa ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
  Wengine ni viungo Simon Msuva, Deus Kaseke, Mkongo Mbuyu Twite, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Matheo Anthony.
  Kinda Yussuf Mhilu aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana, yupo na kikosi cha U-20 Bukoba mkoani Kagera kwenye Ligi Kuu ya Vijana.
  Yanga imeanza mazoezi leo Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam chini ya benchi la jipya lam Ufundi, lililopanuliwa kufuatia ujio wa kocha mpya, Mzambia, George Lwandamina anayechukua nafasi ya Mholanzi, Hans van der Pluijm anayehamia kwenye Ukurugenzi wa Ufundi.
  Na Yanga inajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAKOLANYA AKAMATWA AMEPANDA BODA BODA BILA KUVAA HELMET Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top