• HABARI MPYA

    Sunday, November 20, 2016

    BUSUNGU NA AJALI MBILI MFULULIZO NDANI YA MIEZI MIWILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Yanga, Malimi Busungu jana joni alipata ajali ya pili katika mwezi wa pili mfululizo eneo la Dakawa, Morogoro akiwa njiani kuelekea Dodoma.
    Hata hivyo, bahati nzuri mchezaji huyo hakuumia zaidi ya gari lake aina ya Subaru kuharibika vibaya eneo lote la mbele.
    Meneja wa Busungu, Mohammed Yahya ‘Tostao’ ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kwamba, Busungu ndiye aliyekuwa chanzo cha ajali hiyo baada ya kuligonga gari lililokuwa mbele yake.
    Malimi Busungu baada ya kupata ajali jana joni eneo la Dakawa, Morogoro akiwa njiani kuelekea Dodoma

    “Unajua tena vyombo vya moto hivi, inawezekana gari lake breki zilifeli, basi akaenda kulivaa gari la mwenzake kwa nyuma. Gari la Busungu ndilo lililoumia zaidi, lakini tunashukuru yeye mwenyewe hajaumia, alikuwa analalamika kuumwa tumbo kidogo tu,”alisema Tostao.
    Tostao alisema hiyo ni ajali ya pili mfululizo ndani ya miezi miwili, baada ya mwezi uliopita pia kupata ajali mbaya barabara hiyo, lakini akatoka salama pia.
    Alisema kwa sasa gari zote mbili zinashikiliwa kituo cha Polisi Dakawa kwa uchunguzi zaidi na Busungu amerejea kwao, Mzumbe mjini Morogoro.
    “Yeye nyumbani ni Mzumbe Morogoro, alikuwa ana siku moja tangu afike kutika Dar es Salaam. Dodoma alikuwa anakwenda kwa shughuli zake tu ndiyo bahati mbaya ikawa hivyo,”alisema Tostao. 
    Busungu hajaichezea Yanga tangu Oktoba, baada ya kususua kufuatia kukata tamaa kutokana na kutopewa nafasi ya kucheza chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na alikuwa anashinikiza kuondoka.
    Lakini katikati ya mwezi huu alisema kwamba amesitisha uamuzi wake wa kuondoka Yanga baada ya mabadiliko ya benchi la Ufundi yanayotaka kufanywa na uongozi, Mzambia, George Lwandamina akitarajiwa kuchukua nafasi ya Pluijm.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BUSUNGU NA AJALI MBILI MFULULIZO NDANI YA MIEZI MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top