• HABARI MPYA

    Sunday, November 27, 2016

    KESSY SASA AITOA JASHO SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imetakiwa kuwasilisha vithibitisho vya kumlipa mishahara beki wake, Hassan Ramadhan Kessy katika miezi mitatu ya mwisho kuelekea kumaliza mkataba wake.
    Hiyo inafuatia hoja iliyowasilishwa na Mwanasheria wa Yanga, Alex Mgongolwa leo katika kikao cha Kamati   
    ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji kwamba Simba haina uhalali wa madai yoyote dhidi ya Kessy kwa sababu haikumlipa mishahara kwa miezi mitatu.
    Kikao hicho kilichofanyika makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam jana, Yanga walidai kwamba Simba hawakumlipa mchezaji huyo kwa miezi mitatu kuelekea mwisho wa Mkataba wake na kwa mujibu wa sharia hawana haki ya madai yoyote dhidi yake.
    Habari za ndani kutoka kwenye kikao hicho chini ya Mwenyekiti wa Kamati, Wakili Richard Sinamtwa zinasema kwamba Katibu Mkuu wa Simba SC, Patrick Kahemele aliyeiwakilisha klabu yake leo, ametakiwa kuwa amewasilisha vithibitisho hivyo kesho.
    Beki Hassan Kessy (kushoto) sasa ameanza kuitoa jasho Simba SC

    Na Yanga waliiomba Kamati ipokee vithibitisho vya vielelezo vya kupelekwa mishahara ya Kessy kwenye akaunti yake ya benki na si vinginevyo – kwa kuwa wana wasiwasi wapinzani wao wanaweza kufoji nakala za kumlipa mkononi. 
    Simba inalalamikia klabu ya Yanga kumsajili beki Kessy akiwa hajamaliza mkataba wake Msimbazi na kwa sababu hiyo inataka kulipwa Sh. Milioni 200 ambayo ni punguzo kutoka Bilioni 1.2 walizotaka awali.
    Suala hilo lilianzia Kamati ya Maadili, ambako ilishindikana kupatiwa ufumbuzi na Kamati hiyo ikaagiza Simba na Yanga zikutane zenyewe kumalizana.
    Hata hivyo, mahasimu hao wa jadi katika soka ya Tanzania walishindwa kufikia mwafaka na wakakubaliana kumteua, Mwenyekiti wa zamani wa TFF enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania), Said El Maamry kuwasimamia katika kikao kingine cha kutafuta mwafaka.
    Bahati mbaya, Simba na Yanga mbele ya Mzee El Maamry pia wakashindwa kufikia mwafaka na suala hilo linarudishwa Kamati ya Madili.
    Viongozi wa pande zote mbili, Simba na Yanga wote watakutana mbele ya Kamati ya Maadili iliyo chini ya Mwenyekiti wake,Wakili Richard Sinamtwa kwa kikao cha kulipatia suluhisho suala hilo.
    Kamati hiyo ilisema mapema inawapa nafasi Simba na Yanga wakamalizane wenyewe na ikishindikana, suala hili litarejeshwa Kamati ya Maadili kwa uamuzi.
    Kessy alijiunga na Simba SC mwaka 2014 kutoka Mtibwa Sugar, lakini mapema tu kabla ya kumaliza mwaka wake wa kwanza aliingia kwenye mzozo na klabu hiyo akidai kutokamilishiwa yaliyomo kwenye mkataba, ikiwemo kutopewa nyumba na akagoma.
    Hata hivyo, suala hilo lilitatuliwa na mchezaji huyo akarejea kazini kabla ya kurudi kwenye matatizo tena mwishoni mwa mwaka wake wa mwisho wa mkataba.
    Simba ilimsimamsha mechi tano Kessy kwa tuhuma za kumchezea rafu isiyo ya kimchezo mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher.
    Simba ilifungwa 1-0 na Toto Jumapili ya Aprili 17, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Kessy akatolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu Edward, nyota wa zamani wa timu hiyo Msimbazi.
    Lakini mapema Februari 20, Kessy alianza kupunguza mapenzi ya wana Simba kwake, baada ya kutoa pasi fupi kumrudishia kipa Muivory Coast, Vincent Angban iliyonaswa na mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Ngoma aliyekwenda kuifungia Yanga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0.  
    Iwapo Simba SC itashindwa kuwasilisha vielelezo vya kumlipa mishahara ya miezi ya mwisho wa mkataba wake Kessy, kuna uwezekano madai yao yote yakatupiliwa mbali. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KESSY SASA AITOA JASHO SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top