• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 24, 2016

  MEXIME ASEMA KAGERA SUGAR HAIHITAJI NGUVU MPYA, IPO SAWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA wa Kagera Sugar, Mecky Mexime amesema kwamba hafikirii kuongeza wachezaji katika kikosi chake katika usajili huu wa dirisha dogo, kwa sababu anaamini ana timu nzuri.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo kwa simu kutoka Bukoba, Mexime amesema kwamba hawaoni sababu ya kusajili kwa fasheni zaidi ya kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya timu.
  Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kwamba baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara walijifanyia tathmini na kubaini hawana mapungufu ya wachezaji.
  Mecky Mexime amesema kwamba hafikirii kuongeza wachezaji katika kikosi chake katika usajili huu wa dirisha dogo

  “Sisi tunaona kabisa timu yetu iko vizuri, na baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza tumeona tuelekeze nguvu zetu kwenye maandalizi zaidi, kwani wachezaji tunao wazuri,”amesema beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ya Morogoro.
  Na Mexime amesema timu yake ilianza maandalizi ya Ligi Kuu tangu juzi kambini kwao, Misenyi na wachezaji wote wamekwisharipoti. “Tutakuwa  na mazoezi ya kujenga stamina kwa kipindi chote kilichosalia kumaliza mwezi huu hadi wiki ya kwanza ya Desemba. Baada ya hapo tutaanza mazoezi ya mbinu za mchezo na wiki mbili baadaye tunaweza kucheza mechi za kujipima nguvu,”amesema.
  Kagera Sugar ilimaliza katika nafasi ya nne baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutokana na pointi zake 24 za mechi 15, ikizidiwa pointi 11 na vinara Simba SC.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MEXIME ASEMA KAGERA SUGAR HAIHITAJI NGUVU MPYA, IPO SAWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top